KAMATI YA UCHAGUZI TFF YATUPA RUFANI YA WARUFANI IRFA
Kamati
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana
jana (Septemba 25 mwaka huu) kusikiliza rufani iliyowasilishwa mbele
yake na warufani Mussa H. Mahundi, Abou O. Sillia na Alex Mgongolwa
dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa
(IRFA) iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha matokeo ya
uchaguzi wa IRFA uliofanyika Septemba 8 mwaka huu Mufindi, Iringa, na
kuomba uchaguzi huo ufanyike upya kwa kuendeshwa na kusimamiwa na Kamati
ya Uchaguzi ya TFF.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratias Lyatto,
baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi
ya TFF imejiridhisha kuwa rufani iliyowasilishwa mbele yake na Mahundi,
Sillia na Mgongolwa ilikosa sifa ya kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 8(2), Ibara ya 21(3) na 24(2).
Kwa kutozingatia matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetupa rufani hiyo.
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya IRFA kuchukua hatua
dhidi ya Abuu Changawa kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF, Ibara ya 28(6) kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi wa
IRFA siku ya uchaguzi.
SHUKRANI KWA WADAU SERENGETI BOYS
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru wadau waliofanikisha kwa
njia mbalimbali ziara ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya
miaka 17 (Serengeti Boys) iliyofanyika hivi karibuni katika mikoa ya
Mbeya na Njombe.
Wadau
hao ni Chama cha Mpira wa Miguu Mbeya Mjini (MUFA) chini ya Mwenyekiti
wake Suleiman Haroub, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Njombe (NJOREFA), Stanley Lugenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Mbeya (MREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Njombe (NDFA).
Wengine
ni Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Makambako (MDFA), Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), na klabu za Mbozi United, Kyela
United, Tanzania Prisons na Mbeya City.
Serengeti
Boys inaendelea na kambi yake jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi
ya kwanza ya mchujo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya
miaka 17 dhidi ya Misri itakayochezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment