RAIS wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amefanya mazungumzo
na Rais wa shirikisho la mchezo huo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
kuhusu washambuliaji wa timu ya taifa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.
Wachezaji
hao wamezuiliwa na klabu yao ya TP Mazembe wasirejee kwenye kikosi cha timu ya
taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars ambayo inashiriki michuano ya Kombe la
Chalenji inayoendelea jijini Kampala, Uganda kwa madai kuwa klabu hiyo
inajiandaa kwa mechi za kirafiki baadaye mwezi huu.
Tenga
alifanya mazungumzo hayo na Constanti Omari Selemani , ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) wakati wa ufunguzi wa
michuano ya Kombe la Chalenji jijini Kampala.
Mbali na
mazungumzo hayo, tayari Tenga amemwandikia barua Rais huyo wa Congo akirejea
mazungumzo baina yao juu ya kuwaruhusu washambuliaji hao nyota kujiunga na
Kilimanjaro Stars ambayo imeshashinda mechi moja na kupoteza moja kwenye
michuano ya Kombe la Chalenji.
“Kwa
kuwa kanuni zinaweza kuwa zinaitetea klabu, tunaomba msaaada wako na ufahamu
wako wa masuala ya uongozi wa klabu ili tuweze kupata huduma za wachezaji hawa
wawili kwa ajili ya mashindano haya muhimu kwa nchi yetu na CECAFA (Baraza la
Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati),” inasema sehemu
ya barua hiyo ya Tenga.
Samata
na Ulimwengu walitoa mchango mkubwa kwenye timu wakati Taifa Stars ilipoilaza
Kenya kwa bao 1-0 kaztika mechi ya kirafiki iliyofanyika mapema mwezi huu
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Hata
hivyo kupatikana kwao kuichezea timu ya taifa kumekuwa kwa nadra sana na hivi
karibuni TFF ilieleza kuwa itashughulikia suala la wachezaji hao pamoja na Adam
Nditi anayechezea timu ya vijana ya Chelsea kwa njia ya mazungumzo badala ya
kutumia sheria za FIFA baada ya kushauriwa na vyama vya nchi nyingine vyenye
wachezaji nyota barani Ulaya.
No comments:
Post a Comment