Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeitaka klabu ya Yanga kuwasilisha
maelezo ya ziada na vielelezo kuthibitisha hoja zao dhidi ya mwalimu wa zamani
wa klabu hiyo, Kostadin Papic ambaye ameishtaki klabu hiyo akidai malimbikizo
ya mshahara wake yanayofikia Dola 12,000 za Kimarekani ifikapo Desemba 11, 2012.
Yanga, ambayo ilimuondoa kocha huyo Mserbia mwishoni mwa
msimu wa mwaka 2011/12, inadai kuwa ilishafanya malipo kadhaa, yakiwemo ziada
ya gharama za hoteli aliyokuwa akiishi, na kwamba hadi sasa kocha huyo anadai
si zaidi ya Dola 4,000 za Kimarekani ambazo klabu hiyo imesema itamlipa mara
atakapowasilisha ripoti ya ufundi ya kipindi alichokuwa kocha mkuu.
Katika barua yake kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), FIFA imeitaka Yanga kuwasilisha vielelezo hivyo kabla ya Desemba 11,
2012 baada ya Papic kuliandikia Shirikisho hilo akidai kuwa “haamini kwamba
klabu hiyo itatekeleza ahadi yake ya kulipa deni walilolikubali” na kutaka
kujua itachukua muda gani kulipa baada ya mtaalamu huyo kutoka Serbia
kuwasilisha ripoti yake ya kiufundi kama alivyotakiwa na uongozi wa Yanga.
Katika barua hiyo ambayo imetakiwa iwasilishwe kwenye
uongozi wa Yanga, FIFA imeeleza kuwa kama Yanga haitawasilisha hoja zaidi na
vielelezo ifikapo tarehe hiyo, Shirikisho hilo litachukulia kuwa klabu haina
haja ya kuwasilisha hoja zaidi na hivyo kuendelea na taratibu za kuliwasilisha
suala hilo kwenye Kamati ya Hadhi za Wachezaji kwa ajili ya hatua zaidi na uamuzi
ufanywe kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.
Akizungumzia suala hilo, katibu mkuu wa TFF, Angetilke Osiah
alisema barua hiyo ya FIFA itawasilishwa mapema Yanga ili iweze kujua hatua za
kuchukua kuondoa uwezekanbo wa klabu hiyo kuchukuliwa hatua ambazo zinaweza
kuzuilika.
Yanga pia ilikuwa kwenye hatari ya kushushwa daraja baada ya
kushindwa kuwasilisha vielelezo mapema katika sakata lililomuhusu mchezaji wake
wa zamani, John Njoroge ambaye aliishtaki klabu hiyo FIFA akidai fidia ya
takmriban Sh milioni 17 kutokana na Yanga kuvunja mkataba wake bila ya kufuata
taratibu.
Baada ya kuwasilisha mashtaka yake FIFA, Yanga iliandikiwa
barua iwasilishe utetezi wake lakini ikashindwa kufanya hivyo na kesi hiyo
kusikilizwa upande mmoja na Kitengo cha Usuluhishi cha FIFA (DRC) na kutoa
uamuzi ambao ulimnufaisha beki huyo wa Kenya. Katikati ya mwaka, FIFA ilitoa
agizo la kukazia hukumu hiyo ikitoa siku 30 kwa Yanga kumlipa Njoroge na kwamba
ingeshindwa kufanya hivyo suala hilo lingewasilishwa Kamati ya Nidhamu kwa
ajili ya kuchukua hatua.
Katika barua yake, FIFA ilitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni
kupokonywa pointi, kushushwa daraja au kulipishwa faini kubwa.
No comments:
Post a Comment