Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema
hakuna hila yoyote katika nia ya Shirikisho kutaka marekebisho matatu
kwenye katiba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu na kuwataka wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mabadiliko hayo kwa maslahi ya maendeleo
ya mchezo huo.
Tenga
alisema hayo hii leo wakati akiongea na waandishi wa habari kufafanua juu
ya waraka wa kuomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia
mapendekezo matatu ya mabadiliko ya katiba yanayohusu uingizaji wa
kipengele cha utoaji leseni kwa klabu (Club Licensing); kuundwa kwa
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa TFF na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili
wa Rais wa TFF.
Hatua
ya kutuma waraka wa kuomba ridhaa ya mabadiliko hayo imetafsiriwa
tofauti na baadhi ya wadau, wengine wakisema ni mbinu za uongozi wa sasa
kutaka uendelee kukaa madarakani wakati wengine wakitaka ufafanuzi wa
vipengele hivyo.
“Hakuna
hila hata kidogo. Yote ni mambo ya maendeleo na nia yetu ni kufanikisha
ili mambo yaendelee,”.
“Tusifikie
sehemu tukaanza kulaumu kwa nini mtu ametaka maelezo. Lakini
sikutarajia kuwa mtu wa mpira akiambiwa hili ni agizo la FIFA
(Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu), atasita;
akiambiwa hili ni agizo la CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika),
atasita, au akaambiwa haya ni maamuzi yenu wenyewe, akasita.”
Tenga
alisema kuwa nia ya Kamati ya Utendaji ilikuwa ni kuitisha mkutano mkuu
kwa ajili ya mabadiliko hayo ya katiba, lakini akasema baada ya
kutafakari kwa kina na kuangaliwa uwezo wa Shirikisho, Kamati iliona
haiwezi kuitisha mikutano miwili kwa sasa kwa kuwa TFF haina fedha.
“Tumetoa
maelezo kuwa tunafahamu kuwa katika mazingira ya kawaida tungeitisha
mkutano mkuu; tuje tuzungumze na baadaye siku ya pili watu waondoke
halafu tuwaite tena kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi,” alisema Tenga
ambaye alibainisha kuwa gharama za chini za mkutano mkuu wsa TFF ni kati
ya Sh milioni 90 na Sh milioni 110.
“Lakini
tumeeleza bayana kuwa uwezo huo hatuna, tungelikuwa nao wala
tusingefika mahali hapa; vijana wetu wanahangaika hadi tunatafuta watu
watusaidie. Kwa hiyo tukasema kuna dhambi gani kuwa wa kweli. Katiba
inasema mkitaka kufanya mabadiliko ya katiba, itisheni mkutano mkuu.
Unaita Mkutano Mkuu kwa sababu gani, ili mlete wajumbe wa mkutano mkuu
ambao ndio watakaopitisha mabadiliko hayo na ndio maana tumeona dhana
hiyo ya kutuma waraka.”
Kuhusu
mabadiliko hayo, Tenga alifafanua kuwa maagizo kuhusu utoaji leseni kwa
klabu (Club Licensing) na kuundwa kwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa
TFF yalitolewa mwishoni mwa mwezi Julai, ikiwa ni baada ya kikao cha
Kamati ya Utendaji cha Julai na hivyo suala hilo kulazimika kuzungumzwa
kwenye kikao cha Septemba.
Amesema "Pamoja na kwamba Tanzania ilishaingiza kwenye kanuni za ligi masharti
ya utoaji leseni, CAF imekuja na maagizo kwamba ni lazima itamkwe kwenye
katiba kuwa TFF itatoa leseni kwa klabu kwa mujibu wa maagizo ya CAF na
msipofanya hivyo klabu zenu hazitaruhusiwa kushiriki mashindano ya
klabu ya Afrika ya mwakani,”
Simba
na Azam FC zitaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya
Afrika na Kombe la Shirikisho na hivyo kutopitishwa kwa mabadiliko hayo
mapema kutasababisha wawakilishi wa Tanzania wazuiwe kushiriki michuano
hiyo.
Kuhusu
kuundwa kwa Kamati ya Rufaa, Tenga alisema kuwa baada ya kuomba
ufafanuzi wa utata uliojitokeza katika vyombo vya maamuzi vya TFF, FIFA
ilisema kuwa ili kuondoa mgongano wa kimaslahi, ni muhimu ikaundwa
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa TFF badala ya mfumo wa sasa ambao Kamati
ya Rufaa hujigeuza kuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi inapofikia wakati wa
uchaguzi mkuu wa TFF.
“Kwa
hiyo tunachoomba hapa ni ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba iwepo
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa TFF ili kama mtu hatatendewa haki na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF, basi akate rufaa kwenye Kamati ya Rufaa za
Uchaguzi badala ya chombo kimoja kushughulikia mambo mawili,” alisema
Tenga.
Kuhusu
kuiondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, kiongozi huyo alisema
kuwa suala hilo lilitokana na maamuzi ya Mkutano Mkuu uliopita kuwa
Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza ziendeshwe na chombo huru.
“Baada
ya hapo Kamati ya Utendaji iliziambia klabu kuwa tunaunda Kanuni za
Kuendesha chombo huru cha ligi, tunaomba mapendekezo yenu. Na ndipo
walipotuletea mapendekezo yao kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Ligi atoke
kwenye klabu sita za juu na kwamba kiwango cha chini cha elimu kiwe
Cheti cha Kumaliza Elimu ya Kidato cha Nne kama ilivyo kwenye katiba,”
alisema.
“Maana
yake ni kwamba sifa hizo hazikidhi utashi wa kikatiba wa sifa za
mgombea wa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF ambazo ni Elimu ya
Chuo Kikuu, lakini klabu zikasema hazina haja na nafasi ya Makamu wa
Pili wa Rais na ndio maana tunaomba ridhaa sasa ya kuondoa nafasi hiyo.”
“Napenda
kusema jambo hili ni la maendeleo na hakuna hata moja ambalo si la
maendeleo. Tumepata barua kutoka Kagera ikieleza kuwa utaratibu huu
haufai, Katibu Mkuu amepata na atawajibu. Pwani nao wameomba ufafanuzi
na tutatoa waraka wa ufafanuzi kwa wote.
“Watu
wana haki ya kuhoji na sisi ni wajibu wetu kuwaelimisha. Ombi langu ni
tushirikiane ili twende kwenye mkutano mkuu wetu unaokuja ili
tuchaguane. Tukichaguana tutakuwa tumetimiza jambo muhimu kweli kweli.”
Tenga
pia aliwasihi wajuimbe wa Kamati ya Utendaji kuendelea na jitihada za
kuelimisha wajumbe ili waridhie mabadiliko hayo na shughuli za maendeleo
ya mpira wa miguu ziendelee kama kawaida.
No comments:
Post a Comment