Buriani Chui mweusi , Eusebio da Silva Ferreira, wapenzi wa soka duniani
kote wamlilia mchezaji huyo nyota mzaliwa wa Msumbiji aliyefariki jana
Jumapili(05.01.2014) nchini Ureno.
Eusebio da Silva Perreira , maarufu kama Eusebio ama jina la utani "Chui
mweusi", amefariki jana Jumapili akiwa na umri wa miaka 71, na kifo
chake kimewaletea mashabiki wengi simanzi , wakimkumbuka nyota huyo
ambaye alitokea katika bara la Afrika nchini Msumbiji na kuwa mmoja kati
ya wachezaji nyota duniani.
Eusebio aliyefariki siku ya Jumapili asubuhi kutokana na moyo wake
kushindwa kufanyakazi, alitawala soka nchini Ureno katika miaka ya 1960,
na kuiletea sifa nchi hiyo pamoja na klabu yake ya Benfica Lisbon.
Serikali ya Ureno imetangaza siku tatu za maombolezo, na bendera mjini
Lisbon zinapepea nusu mlingoti kabla ya mazishi yake siku ya Jumatatu
ambapo mamia kwa maelfu ya watu wanatarajiwa kujipanga mitaani kutoa
heshima zao za mwisho.
Wachezaji kadha wa zamani ikiwa ni pamoja na Bobby Chalton ambaye
aliisaidia Manchester United kupata ushindi dhidi ya Benfica katika
mwaka 1968 katika fainali ya kombe la Ulaya ambalo sasa ni champions
League , amesema ilikuwa ni nafasi ya pekee kumfahamu Eusebio. Franz
Beckenbeuer nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani katika kombe la dunia
1970 , 74 na 78 amemueleza Eusebio kama rafiki yake na nyota wa wakati
huo.
Kwa wengi Eusebio aliyezaliwa mwaka 1942 nchini Msumbiji hadi leo hii
ndie mchezaji bora kabisa katika historia ya soka nchini Ureno na
mchezaji wa kwanza nyota kutoka bara la Afrika. Ameisaidia timu yake ya
Benfica kupata mafanikio kadha kitaifa na kimataifa. Mwandishi wa habari
za michezo mzaliwa wa Msumbiji Jose Musuaili alimpenda sana Eusebio
tangu akiwa mtoto , licha ya kuwa yeye binafsi alikuwa shabiki mkubwa wa
timu hasimu nchini Ureno ya Sporting Lisbon.
"Alikuwa kipenzi cha kizazi chote cha baba zetu. Na hata leo ni alama
maalum kwetu. Sio tu kwa wapenzi wa soka kwa sisi Waafrika, lakini pia
kwa watu wote, ambao wanazungumza lugha ya Kireno. Nimebahatika, kuwa
rafiki wa familia ya Eusebio. Katika mahojiano yangu ya kwanza na
Eusebio , nilitambua kuwa Eusebio kwa kweli yuko kama tunavyomuona. Kwa
upande mmoja ni nyota wa soka la Ureno na kimataifa, lakini kwa upande
mwingine ni mtu wa kawaida kabisa."
Eusebio akifunga bao
Eusebio aliichezea Ureno mara 64 alifunga mabao 41. Pia alituzwa kiatu
cha dhahabu mara mbili na amekuwa mfungaji bora nchini Ureno kati ya
mwaka 1964 na 1973. Aliipatia ushindi wa ligi Benfica mara 11 pamoja na
vikombe vitano vya chama cha mpira nchini Ureno. Aliistaafu soka mwaka
1979. Mungu amlaze mahali pema . Ameen.
No comments:
Post a Comment