Leo hii ni siku ya kwanza kazini kwa makocha Charles Bonface Mkwasa 'Master' na Juma Pondamali 'Mensa' tangu wachukue ajira mpya ya kukinoa kikosi cha Yanga ambacho ninaongoza ligi kuu ya Tanzania huku pia wakiwa ni watetezi wa kombe la ligi hiyo.
Makocha hao wanajukumu la kubadilisha hali ya ubora wa soka la timu hiyo kuleta matumaini mapya kwa mashabiki wa Yanga ambao kwasasa wana kumbukumbu ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa watani zao wakubwa katika soka la Tanzania Simba SC katika mchezo wa kirafiki wa Mtani Jembe uliandaliwa na wadhamini wa vilabu hivyo kampuni ya Safari Lager Disemba 21 mwaka jana.
Mkwasa alichukua nafasi ya Freddy Felix Minziro maarufu kama 'baba Isaya-Majeshi' katika nafasi ya kocha msaidizi ilhali Juma Pondamali maarufu kama 'Mensar' akichukua nafasi ya Razaki Siwa wote walikatishiwa mikataba yao bila sababu za msingi kuelezwa na klabu hiyo.
Yanga kwasasa inasubiri kukamilisha banchi lake la ufundi kwa nafasi ya kocha mkuu ambaye bado haijajulikana kuwa atakuwa ni nani licha ya klabu hiyo kudai kuwa imekuwa ikipokea maombi lukuki kutoka ndani na nje ya nchi kutoka kwa makocha mbalimbali ambao wanataka kuziba pengo la kocha mzungu raia wa Uholanzi aliyetimuliwa kazi Ernie Brandts mwezi Disemba.
Yanga licha ya kuwa na wachezaji wengi nyota kutoka katika ukanda wa Afrika mashariki na kati na wengine wenye vipaji vya hali ya juu kutoka nchini Tanzania, bado imeendelea kuonyesha soka bovu uwanjani licha ya kuongoza ligi kuu ya soka Tanzania bara huku wachezaji wakionekana kuchezo kibinafsi na si kwa nidhamu ya kitimu.
Hivi karibuni Yanga ilifanikiwa kumsajili mshambuliaji nyota wa Uganda Emmanuel Okwi kutoka SC villa ya Uganda ambaye kabla ya kuichezea Villa alikuwa nchini Tunisia katika klabu ya Etoile Du Sahel ambayo alijiunga nayo baada ya kuuzwa huko na watani zao Simba.
Yanga ilisimama kufanya mazoezi kwa siku takribani tatu
kufuatia kufanya mabadiliko ya benchi la Ufundi na leo rasmi imeanza
mazoezi asubuhi chini ya makocha hao wapya.
Mkwasa alitumia muda wa dakika 5 kuongea na wachezaji
wote waliofika mazoezini siku ya leo, kuwaelekeza nini wanapaswa kufanya
na kuzingatia mafunzo yake ambapo wachezaji waliweze kutekeleza kwa
kiwango cha hali ya juu.
Kocha wa makipa Juma Pondamali aliwafua
vilivyo magolikipa Juma Kaseja, Ally Mustafa "Barthez" na Deogratias
Munish "Dida" na kusema huu ni mwanzo tu kwani anaamini wachezaji hao
watakua katika kiwango kizuri kutokana na uwezo wanaouonyesha katika
mazoezi anayaowapatia.
Kikosi cha Young Africans kesho kitaendelea
na mazoezi asubuhi katika uwanja wa Mabatini Kijitonyama ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya mzunguko wa pili na mashindano ya kimataifa.
Aidha
washambuliaji Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi waliokwenda kwao nchini
Uganda kwa ajili ya matatizo ya kifamilia wanatarajiwa kurejea nchini
mwishoni mwa wiki tayari kuungana na wenzao kujiandaa na mzunguko wa
pili.
No comments:
Post a Comment