Young Africans imemkaribisha vizuri kocha mkuu mpya Hans Van Der Plyum
leo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Altay SK
iliyopo Ligi Daraja la pili nchini Uturuki katika mchezo wa kirafiki wa
kimataifa uliofanyika leo mchana katika viwanja vya Sueno eneo la Side
Manavgat.
Kocha Hans ambaye aliwasili jana jioni na kuongea na wachezaji kwa
pamoja kabla ya chakula cha usiku alisisitiza nidhamu, upendo na
kujituma miongoni mwa wachezaji na benchi la ufundi kitu ambacho mpaka
sasa amefurahishwa na ushirikiano anaopewa na wachezaji na viongozi kwa
ujumla.
Ikiwa mechi yake ya kwanza kama kocha mkuu wa Young
Africans Hans aliweza kukaa kwenye benchi pamoja na makocha Charles
Mkwasa, Juma Pondamali, Hafidh Saleh na daktari wa timu Dr. Suphian Juma
ambapo kwa pamoja kikosi kimeweza kuendeleza ushindi wa pili mfululizo.
Mechi
ilianza kwa kasi kwa timu zote kusaka mabao ya mapema, lakini umakini
wa walinzi wa timu zote mbili ilikuwa kikwazo kwa washmbuliaji wa timu
zote kuweza kupata mabao kwani mipira yao mingi iliishia kuchezwa na
walinzi na walinda milnago wa timu zote.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika matokeo yalikuwa suluhu.
Kipindi
cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 46 ya mchezo, mshambuliaji
Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao la kwanza baada ya
kuitumia vizuri pasi ya kiungo Haruna Niyonzima na kuwatoka walinzi wa
Altay na kumchambua golikipa wao na kuhasabu bao la kwanza kwa watoto wa
jangwani.
Mara baada ya bao hilo, Altay walicharuka na kufanya
mashambulizi ya nguvu ya kusaka bao la kusawazisha lakini mlinda mlango
Ally Mustafa "Barthez" alifanya kazi ya ziada kuokoa mipira miwili ya
wazi iliyokuwa inaelekea wavuni na kuwa kona ambazo hazikuzaa matunda.
Dakika
ya 57 ya mchezo mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Uganda Emmanuel
Okwi aliipatia Young Africans bao la pili na la ushindi baada ya
kupokea pasi safi ya kiungo Haruna Niyonzima kabla ya mganda huyo
kuukwamisha mpira wavuni na kuhesabu bao la pili.
Frank Domayo
alikosa nafasi mbili za wazi za kufunga baada ya mashuti aliyopiga kupaa
sentimite chache juu ya lango la Altay huku Hamsi Kiiza akikosa bao la
wazi bada ya mpira alioupiga kugonga mwamba na kurudi uwanjani.
Hamis
Kiiza alikosa penati dakika ya 83 ya mchezo baada ya mchomo wake
kupanguliwa na mlinda mlango wa Altay SK kabla ya Kiiza tena kuuwahi
kuumalizia na kutoka juu ya lango la Altay SK.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Altay SK 0 - 2 Young Africans
Kocha
mkuu mpya wa Young Africans mholanzi Hans Van Der Plyum amesema timu
yake imecheza vizuri na hasa kipindi cha pili, kwani kipindi cha kwanza
wapinzani waliwaabana sana na kushindwa kupata bao lakini kipindi cha
pili washambuliaji wake walitumia vizuri nafasi walizozipata na ndio
maana timu ikapata ushindi.
"Huu ni mwanzo mzuri tupo hapa Uturuki
kwa ajili ya kambi ya mafunzo, wachezaji wamecheza vizuri kwa kipindi
hiki kilichobakia kabla ya kurejea Tanzania tutaendelea kuwaandaa vijana
wake katika uwezo mzuri na tayari kwa Ligi Kuu na mashindano ya
kimataifa" alisema Hans
Mara baada ya mechi ya leo timu itaendelea
na mazoezi kesho asubuhi kuendelea kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom na
mashindano ya kimataifa.
Young Africans: 1.Ally
Mustafa "Barthez", 2.Juma Abdul, 3.Oscar Joshua/David Luhende, 4.Mbuyu
Twite, 5.Kelvin Yondani, 6.Frank Domayo, 7.Haruna Niyonzima, 8.Hassan
Dilunga/Nizar Khalfani, 9.Didier Kavumbagu/Hamis Kiiza, 10.Emmanuel
Okwi, 11.Mrisho Ngasa/Saimon Msuva
No comments:
Post a Comment