Mohamed Bhinda akiwa na makamu mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga wakitete jambo. |
Viongozi wa
matawi ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati ama mabingwa watetezi wa kombe
la Kagame Yanga hii wamemgomea mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo Mohamed
Bhinda kuketi katika meza kuu ya viongozi wa klabu hiyo wakati wa mkutano wa
hii leo ulioitishwa na makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Clement Sanga.
Mkutano huo ulioitishwa
na Sanga ulikuwa na lengo la kupanga mikakati ya timu ya Yanga kutetea kombe la
michuano ya Kagame kufuatia timu hiyo kufanikiwa kutinga katika hatua ya nusu fainali
ya michuano hiyo inayo endelea hivi sasa jijini Dar es Salaam na kesho
wakikabiliwa na mchezo wa nusu fainali dhidi ya mabingwa wa soka wa Rwanda APR.
Katika
mkutano huo wanachama wa Yanga waligoma katakata kumruhusu Bhinda kukaa meza
kuu mzozo ambao ulichukua takribani saa nzima huku jitihada za makamu
mwenyekiti Clement Sanga zikionekana kugonga mwamba.
Wanachama
hao walikuwa wakitoa hoja kuwa Bhinda alikuwa ni msaliti katika kipindi cha uongozi
wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu wakati huo Lyod Nchunga ambapo viongozi
wenzake walikubali wakijiuzulu kwa shinikizo la wanachama wa klabu hiyo lakini
yeye alitangaza kufanya hivyo mbele ya wanachama kisha baadaye akarejea
kutokana na kutokuwepo na taarifa ya kujiuzulu kwake kimaandishi.
Sakata la
leo lilikuwa kubwa lakini hatimaye busara ikatawala kikao hicho kwa jitihata za
ziada za makamu Sanga ndipo viongozi hao
wa matawi walipomruhusu kwa shingo
upande kuketi katika meza hiyo.
Mbali na
Bhinda mwingine aliyekutana na kadhia hiyo ni ni mwenyekiti wa matawi wa mkoa
wa Dar es Salaam Mohamed Msumi ambaye alitakiwa kuondoka kabisa meza kuu kwa
dhana ya muda wake wa uongozi kuwa umekwisha lakini akaokolewa na kura za
viongozi hao wa matawi kujiridhisha kuwa muda wake bado unaendelea.
Viongozi hao
wa matawi wamekubaliana kimsingi kuunganisha nguvu zao katika michezo ya nusu
fainali na fainali ya kombe la Kagame endapo timu hiyo itafanikiwa kuifunga APR
katika mchezo wa kesho uwanja wa taifa huku mchezo mwingine wa hatua hiyo
mchana saa nane utakuwa ni baina ya Azam na Vita Club ya DRC.
No comments:
Post a Comment