KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Friday, August 31, 2012

KUTOKA TFF:MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI SEPT 27,SERENGETI BOYS KUJIPIMA KWA ASHANTI NA MCHEZAJI WA MTIBWA SUGAR NAYE APATA ITC AYOUB HASSAN ISIKO WA BULL FC.


MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI SEPT 27
Mtihani kwa ajili ya watu wanaotaka kuwa mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Septemba 27 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa wanaotaka uwakala huo wanatakiwa kujisajili ambapo watapewa kanuni mbalimbali za FIFA na TFF ili waweze kujiandaa kikamilifu kwa mtihani huo utakaokuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka TFF. Ada ya mtihani ni dola 50 za Marekani.

Pia Damas Ndumbaro na Ally Mleh wa Manyara Sports Management ambao tayari ni mawakala wanaotambuliwa na FIFA wanatakiwa kufanya mtihani huo kama wanataka kuendelea na uwakala kwa vile muda wa leseni zao za awali umemalizika.

Mawakala wengine ambao ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully leseni zao bado ziko hai.


SERENGETI BOYS KUJIPIMA KWA ASHANTI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyokuwa kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya itavunja rasmi kambi yake kesho (Jumamosi) kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ashanti United.
Mechi hiyo dhidi ya Ashanti United iliyoko daraja la kwanza itachezwa kuanzia saa 10 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh. 2,000.
 Serengeti Boys ilikuwa Septemba 9 mwaka huu icheze na Kenya kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, lakini Kenya ikajitoa ambapo sasa itacheza na Misri katika raundi ya pili. Mechi ya kwanza itachezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mwishoni mwa Septemba, Serengeti Boys itarejea tena kambini kujiandaa kuikabili Misri ambapo kabla inatarajia kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu itakayotangazwa baadaye.

MCHEZAJI WA MTIBWA SUGAR NAYE APATA ITC


Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) limetuma Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na Mtibwa Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.

ITC hiyo ilitumwa jana (Agosti 30 mwaka huu), hivyo kufanya wachezaji ambao ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu. Dirisha la usajili wa wachezaji litafungwa rasmi Septemba 4 mwaka huu.

Wachezaji ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba. ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati wowote kwani tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.

 Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 

No comments:

Post a Comment