KLABU ya Yanga na Kocha Msaidizi wa timu ya Toto
Africans, Athuman Bilali wamepigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kutokana na
makosa mbalimbali katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea
nchini.
Adhabu hizo zimetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili (Aprili 7 mwaka huu)
jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za waamuzi na makamishna kwa michezo namba
108 hadi 171.
Yanga imepigwa faini hiyo baada ya kupata kadi tano za
njano katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Februari 7 mwaka huu.
Vilevile Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye
kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) dhidi ya African Lyon
iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu.
Naye Kocha Bilali amepigwa faini hiyo na kufungiwa
mechi tatu za ligi hiyo kwa kumshambulia kwa maneno kocha wa timu pinzani, hali
iliyosababisha mwamuzi amtoe kwenye benchi la wachezaji. Alifanya tukio hilo
kwenye mechi kati ya Toto Africans na Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3
mwaka huu jijini Mwanza.
African Lyon na Simba zimepigwa faini ya sh. 500,000
kila moja kwa kushindwa kuchezesha timu zao za U20 kwenye mechi za utangulizi
wakati zilipocheza na Oljoro JKT na Coastal Union, Machi mwaka huu kwenye
viwanja vya Azam Complex na Uwanja wa Taifa.
Suala la Meneja wa Coastal Union, Akida Manchai
kumshambulia kwa maneno yasiyo ya kiungwana Makamu Mwenyekiti wake Steven
Mnguto baada ya kwenye mechi kati ya African Lyon na Coastal Union iliyochezwa
Machi 30 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex limepelekwa Kamati ya Nidhamu kwa
ajili ya hatua za kinidhamu.
Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi
Kuu ya Vodacom.
No comments:
Post a Comment