Polisi Morogoro inapambana na Ruvu Shooting katika
moja kati ya mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa kesho
(Aprili 10 mwaka huu). Matokeo ya mechi hiyo yanatarajia kutoa mwanga kama
Polisi inaweza kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Timu hiyo itakuwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro katika mechi hiyo itakayochezeshwa na Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga
akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Ephrony Ndissa wa Arusha.
Polisi Morogoro inayonolewa na Adolf Rishard inakamata
nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 18 tu na imebakiza mechi tatu dhidi ya Simba,
Kagera Sugar na Coastal Union.
Mechi nyingine za kesho ni kati ya Tanzania Prisons
iliyo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 20 dhidi ya Mgambo Shooting. Mwamuzi Hashim
Abdallah wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi hiyo kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Mgambo ina pointi 24 na iko katika nafasi
ya tisa.
Mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam atachezesha mechi
kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Toto Africans itakayofanyika Uwanja wa Manungu
ulioko Turiani mkoani Morogoro. Toto Africans ya Kocha John Tegete ina pointi
21 ikiwa nafasi ya 11 wakati Mtibwa Sugar iko nafasi ya tano na pointi zake 32.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili 11 mwaka huu)
kwa mechi moja kati ya Azam na African Lyon itakayofanyika Uwanja wa Azam
Complex.
No comments:
Post a Comment