Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ya Polisi
Tabora, Regan Mbuta kilichotokea jana (Machi 31 mwaka huu) usiku kwa
ajali ya pikipiki mjini Tabora.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora
(TAREFA), Yusuf Kitumbo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo (Aprili 1
mwaka huu) kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani
Morogoro kwa ajili ya maziko.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mbuta alikuwa mmoja wa
washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao lake la mwisho
aliyoifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu huu dhidi
ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta, TAREFA na klabu ya Polisi
Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mbuta mahali
pema peponi. Amina
No comments:
Post a Comment