Na Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
TIKETI MECHI YA STARS KUANZA KUUZWA KESHO
Wakati
timu ya Ivory Coast inatarajiwa kuwasili leo usiku (Juni 13 mwaka huu)
kwa ndege maalum, tiketi kwa ajili ya mechi kati yake na Taifa Stars
itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa zinaanza kuuzwa kesho
mchana (Juni 14 mwaka huu) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Vituo
vitakavyotumika kwa mauzo hayo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa,
Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom
Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Salon iliyoko
Sinza Madukani.
Viingilio
katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika
kundi C ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani, sh. 7,000 viti vya
rangi ya bluu, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C,
sh. 20,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Pia
viti 100 vilivyo katika sehemu ya Wageni Maalumu (VVIP) vitauzwa kwa
sh. 50,000 kila kimoja. Tiketi hizo zitauzwa katika ofisi za TFF, na
watakaonunua watapewa kadi maalumu zenye majina yao, majina ambayo pia
watayakuta katika vita watakavyokaa. Kwa maana hiyo hakutakuwa pasi
maalumu (free pass) za kuingia VVIP.
PONGEZI KWA RAIS MPYA WA ZFA
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amempongeza Rais mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Ravia
Idarous Faina aliyechaguliwa katika uchaguzo mdogo uliofanyika hivi
karibuni.
Amesema
ushindi aliopata Faina unaonyesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA
walivyo na imani naye katika kuhakikisha maendeleo ya mpira wa miguu
visiwani humo.
Rais
Tenga amesema ni imani yake kuwa Rais Faina ataendeleza ushirikiano
uliopo kati ya TFF na ZFA kwa ajili ya ustawi wa mpira wa miguu katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumtakiwa kila kheri katika wadhifa
wake huo mpya.
WAAMUZI WATATU WAFUNGIWA MIEZI MITATU
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefungia miezi mitatu waamuzi watatu
walioshindwa kuchezesha mechi namba 32 ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa
(RCL) kati ya Mpwapwa Stars ya Dodoma na Machava FC ya Kilimanjaro
iliyokuwa ichezwe Juni 2 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
TFF
kupitia Kamati yake ya Waamuzi iliyokutana katika kikao chake cha Juni
12 mwaka huu kupitia taarifa mbalimbali za waamuzi wa RCL ilibaini
makosa yaliyofanywa na baadhi ya waamuzi na kuyatolea uamuzi.
Waamuzi
hao waliofungiwa ambao wanatoka mkoani Singida ni Jilili Abdallah,
Amani Mwaipaja na Theofil Tegamisho. Wamefungiwa kwa kutoripoti katika
kituo walichopangiwa (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma) na kutoa taarifa ya
uongo kwa kushirikiana na Kamishna wa mechi hiyo.
Kanuni
iliyotumika kuwafungia ni ya 28 kifungu (d) na (g) ya Ligi za TFF, na
adhabu hiyo imeanza Juni 13 mwaka huu. Waamuzi hao pamoja na kamishna
badala ya kwenda Uwanja wa Jamhuri, wao walikwenda kwenye Uwanja wa
Mgambo ulioko Mpwapwa na kuandika ripoti iliyoonesha kuwa timu ya
Machava FC haikufika uwanjani wakati wakijua kuwa mechi hiyo ilitakiwa
kuchezwa katika Uwanja wa Jamhuri.
No comments:
Post a Comment