Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema
hakuna hila yoyote katika marekebisho ya Katiba kwa vile yametokana na
maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Akizungumza
na Wahariri wa Michezo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Julai 9
mwaka huu), Rais Tenga amewahakikishia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
Dharura kuwa dhamira ya marekebisho hayo ni nzuri, kwani lengo ni kila
mtu apate haki yake.
Amesema
Mkutano huo utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) utakuwa na
ajenda moja tu ya kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya
Maadili katika Katiba ya TFF kama ilivyoelekezwa na FIFA ili baadaye
uanze mchakato wa uchaguzi.
“Katika
kuunda Kamati ya Maadili tumeangalia ile ile ya FIFA, tusitengeneze
kitu kipya, yaondolewe yale yanayotakiwa kuondolewa, na yaongezwe yale
yanayotakiwa kuongozwa. Kwa sababu tumeangalia mazingira kwa Tanzania ni
tofauti na Ujerumani au nchi za sehemu zingine,” amesema.
Rais
Tenga amewataka wajumbe wafike kwenye Mkutano wakiwa na mtazamo wa
kujenga, kwani kuna maagizo ya FIFA ambayo wanatakiwa kuyatekeleza ili
wasonge mbele.
“Tutawaeleza
kwanini hili limewekwa na lile limeondolewa. Mpira unataka unit (kitu
kimoja), ni mchezo wa kila mtu. Baada ya hapa tunaanzisha mchakato wa
uchaguzi. Watu wanaingia wakiwa wamoja, wanatoa hoja wanasikilizwa.
Wanahukumiwa kwa hoja,” amesema na kuongeza utatolewa muda wa kutosha
wajumbe ili wayaone na kuelewa marekebisho hayo.
Rais
Tenga pia alizungumzia kipindi hiki cha usajili na kutaka klabu
ziwaachie wataalamu wa mpira wa miguu kwani ndiyo wanaojua upungufu wa
timu, hivyo wanaweza kusajili wachezaji sahihi.
Amesema
tatizo kubwa la klabu za Tanzania ni kuwa timu zao hazina uwezo wa
kuhimili dakika 90, hivyo watu wanapaswa pia kuzungumzia aina ya mazoezi
ambayo timu zao zinafanya badala ya kubakia kutaja tu majina ya
wachezaji wanaotaka kusajiliwa.
No comments:
Post a Comment