Wakati mamilioni
ya Watanzania wakifuatilia Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, Shirika la
kutetea haki za watoto la Plan International limeingia ubia na Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi
wa haki za mtoto hapa nchini.
Kwa lengo hilo,
mkataba wa ushirikiano umesainiwa leo katika ofisi za makao makuu ya TFF jijini
Dar es Salaam baina ya Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen
Haldorsen na Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Ushirikiano huo unalenga kufanya kazi pamoja
katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa
Haldorsen, mchezo wa mpira ndio unaoongoza nchini na kote duniani kwa kuwa na ushabiki
mkubwa na kwamba joto kali juu ya Fainali za Kombe la Dunia linaloendelea
Brazil ni ushahidi tosha.
“Tunatambua
uwezo wa mchezo huu wa kuwajumuisha watu. Sasa tunataka tuwajumuishe watu sio tu
kwa ajili ya furaha lakini pia kama njia ya kuleta mabadiliko juu ya usawa wa kijinsia
kwa kutetea na kuhamasisha juu ya haki za mtoto wa kike,” aliongeza.
Mkurugenzi
huyo alidokeza kuwa ushirikiano na TFF ni sehemu ya kampeni ya kimataifa inayoendeshwa
na shirika hilo kote ulimwenguni inayoitwa ‘Because I Am A Girl’-BIAAG au kwa
Kiswahili- KWA SABABU MIMI NI MSICHANA ambayo inalenga kuwatoa mamilioni ya wasichana
kutoka katika umaskini kupitia uhamasishaji juu ya haki zao, elimu na stadi za maisha.
“Kwa kupitia
ubia huu tutakuwa na uwezo wa kuwafikia mamilioni ya Watanzania na tutawapa wasichana
ujumbe kuwa KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima nipate fursa sawa na wavulana.
KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima niwe na uwezo wa kufunga magoli ya kufikia ndoto
zangu katika maisha,” Haldorsen alieleza.
Kwa upande
wake, Rais wa TFF, ambaye ni mjumbe katika Kamati ya Huduma kwa Jamii ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni- FIFA, alisema kuwa
ubia huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za huduma kwa jamii ya TFF na kwamba wana
furaha kushirikiana na Plan International kwa lengo hili muhimu.
“Ushirikiano
huu ni muhimu sana kwetu kwani unakileta chombo kikubwa kabisa cha michezo hapa
nchini pamoja na shirika la Plan International hususan kwa ajili ya haki za mtoto
wa kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu nchi nzima kuelimisha juu ya usawa wa
kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto wa kike,” alisema Rais Malinzi.
Kwa pamoja tutashughulikia
masuala ya usawa wa kijinsia, hususan kupambana na ndoa za utotoni ambazo zinawazuia
mamilioni ya watoto wa kike nchini wasiweze kumaliza shule, kufikia ndoto zao katika
maisha, na vile vile kuwaacha waendelee kuteseka katika umaskini,” Rais Malinzi
aliongeza.
KUHUSU PLAN INTERNATIONAL: Plan
International ni shirika la kimaendeleo la misaada ya kibinadamu, linalomlenga mtoto
lisilofungamana na mrengo wowote wa kidini, kisiasa au kiserikali.
Plan
International ilianzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita na inaendesha shughuli zake
katika nchi 70 duniani. Plan International imekuwa inafanyakazi hapa Tanzania
tangu mwaka 1991 ikiwasaidia watoto na jamii kupata huduma za afya, elimu,
maji, usafi na mazingira, kujikimu na ulinzi. Inaendesha miradi Dar es Salaam,
Morogoro, Dodoma, Geita, Pwani, Mwanza na Rukwa.
KAMPENI YA KWA SABABU MIMI NI
MSICHANA –BIAAG: Kampeni ya Kwa Sababu Mimi ni Msichana-BIAAG (2012-2016)
ni kampeni ya Plan ulimwenguni kote inayolenga kuelimisha na kutetea haki za mtoto
wa kike na kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka kwenye lindi la umaskini kupitia
elimu na utoaji wa stadi za maisha na kazi.
Kampeni hii
inalenga kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana milioni
4 duniani na zaidi ya laki 3 hapa Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga shuleni,
kupata stadi za kiufundi na maisha, kujikimu, na kushiriki katika shughuli mbalimbali
katika jamii na kulindwa, kwa kukabiliana na vikwazo dhidi ya maendeleo ya mtoto
wa kike.
No comments:
Post a Comment