Marcio Maximo kubaki Pemba ilhali Neiva akielekea Kigali kwa michuano ya Kagame |
Kuelekea katika michuano ya kombe la kagame nchini Rwanda
Kocha mkuu wa Yanga M-brazil Marcio Maximo ameamua kuigawa timu yake katika
makundi mawili ya kombe la Kagame na kingine ambacho kitapiga kambi
huko Pemba kuendelea na maandalizi ya ligi ya soka Tanzania Bara pamoja na kombe la shirikisho.
Akiongea na waandishi wa habari shule ya sekondari ya Loyola
ambako mazoezi ya kikosi chake hufanyika, Maximo amesema ameamua kufanya hivyo
kwa lengo la kuwajua zaidi wachezaji wake na kujenga usawa wa mapokeo ya mafunzo yake lakini pia kusaka
kikosi cha kwanza.
Maximo ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja majina ya
wachezaji wa makundi hayo kwa kile alichosema muda bado wa kufanya hivyo
ametanabaisha kuwa kikosi cha Pemba kitakuwa chini yake na kile kitakacho
kwenda katika michuano ya Kagame kitakuwa chini ya msaidizi wake Leonardo Neiva.
Maximo amesema kwake makundi yote ni muhimu na kwamba wale watakao kuwa katika kundi la michuano ya Kagame watakuwa ni wale ambao anawajua vema kwani alikuwa nao katika mazoezi katika kipindi chote cha mazoezi tangu alipowasili nchini.
Maximo amesema anategemea kupata taarifa sahihi kutoka kwa msaidizi wake Neiva kutoka Rwanda juu ya namna wachezaji wake walivyofanya huko.
Maximo pia amesema atawatumia wachezaji wengi wa kikosi cha pili huko Rwanda kwani hiyo ni nafasi ya kuwapa changamoto wachezaji hao ambao mara nyingi imekuwa ni rahisi kuwazungumzia kuliko kuwapa nafasi ya kucheza.
Aidha amesema pamoja na wachezaji wengine atakao salia nao pia atabaki na wachezaji waliokuwa katika vikosi vya timu za taifa kwa lengo la kuwajua zaidi viwango vyao kwani tangu alipowasili nchini hakupata nafasi ya kuwaona.
No comments:
Post a Comment