KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Monday, August 11, 2014

MAMBO YA KUJIULIZA BAADA YA KUTIMULIWA KAZI KWA KOCHA ZDRAVKO LOGARUSIC

Kikosi cha Simba kilichoshuka dimbani dhidi ya ZESCO siku ya Simba Day, kulia ni kocha aliyetimuliwa kazi Logarusic Zdravko na kushoto ni bosi wa Simba Rais Evance Aveva aliyemtimua kazi Logarusic
Wakati uongozi wa Simba ukitangaza kumfuta kazi Zdravko Logarusic yapo mambo kadhaa ya kujiuliza kufuatia uongozi wa klabu Simba kumtimua kazi kocha Zdravko Logarusic ikiwa ni siku 18 zimepita tangu kuingia mkataba wa mwaka mmoja.

Uongozi wa Simba kupitia kwa makamu wa Rais wa klabu hiyo ulikaririwa ukisema kuwa mkataba huo mpya kwa Loga umefuatia uongozi huo kuridhishwa na utendaji wake wa kazi katika kipindi chake cha awali cha mkataba wa miezi sita kukamilika ambapo aliichukua kazi hiyo kwa watangulizi wake Abdalah King Kibadeni Mputa na Jamhuri Kihwelu timu ikiwa katika nafasi ya nne na kumaliza msimu uliopita wa ligi katika nafasi hiyohiyo ya nne.
Rais  wa Simba Evance Aveva akionyesha vidole vitatu kabla ya uchanguzi wa Simba uliofanyika mwezi juni
Logarusic alikabidhiwa vikosi vyote viwili, kile cha timu kubwa na ile ya vijana akisadiana na kocha wa kizalendo Selemani Matola huku uongozi huo ukiahidi ya kwamba hautakuwa tayari kumuingilia katika kazi yake.

Maswali ni mengi yakujiuliza ndani ya kipindi hiki kifupi baada ya kumuongezea mkataba huo Loga, uongozi huo unaibuka mbele ya umma wa watanzania na kutangaza kuuvunja mkataba huo ikiwa ni siku moja tu kupita (kama sio masaa) baada ya utambulisho wa kocha huyo na kikosi kizima cha wachezaji katika siku kubwa ya wana Simba (yaani Simba day) ambapo Simba ilicheza na ZESCO ya Zambia na kufungwa 3-0 uwanja wa Taifa jijini Dar  es Salaam.

Natambua wazi kuwa Simba bado haijakamilisha usajili wake, lakini pia imekuwa bado inawajaribu wachezaji kadhaa kabla ya kutangaza usajili kamili huku tarehe ya mwisho iliyotangazwa na shirikisho la soka nchini TFF ya kufunga dirisha la usajili ikiwa ni Agosti 17 2014, na ligi kuu ya soka Tanzania bara ikitarajiwa kuanza Septemba 20 2014.

Tukirejea mkataba wa Simba la Logarusic ni sahihi kabisa kwamba kipo kifungu ambacho kinaelezea ni kwa namna gani mkataba huo unaweza kuvunjwa endapo pande hizo mbili zitashindwa kuafikiana katika mambo fulani ndani ya mkataba huo.

Kichwa kinazidi kuumia kwa kuwa uongozi huo wa Simba mbali na kutoa sababu ya kwamba wamekuwa wakijadiliana na kocha Logarusic katika kujaribu kuwekana sana lakini bila ya mafanikio hakukuwa na nafuu yoyote iliyonekana hivyo wameamua kuuvunja mkataba huo kwa manufaa ya Simba.

Swali ni mambo gani hayo ambayo mmeshindwa kufikia muafaka baina yenu kiasi kutoa maamuzi hayo magumu, lakini pia kumbukeni Uongozi mpya wa Simba tangu mlipoingia madarakani mwezi Julai mosi uongozi wenu bado hauja unda kamati ya ufundi ambayo pengine ingewaongoza katika kuwasiliana na benchi la ufundi chini ya kocha Logarusic akisaidiwa na Matola.

Kamati mliyounda ni ya usajili chini ya Zacharia Hans Poppe akisaidiwa na Kassim Mohammed Dewji na wajumbe ni Said Tuliy, Musley Al Ruwaih, Crescentius Magori na Dk Roadney Chiduo
Zitabaki kumbukumbu za Logarusic
Kamati ngingine mliyounda ni ya Soka ya Vijana iliyo chini ya Mwenyekiti Said Tuliy akisaidiwa na Ally Suru, Patrick Rweyemamu, Mulamu Nghambi, Madaraka Suleiman na Amina Poyo.

Nyingine ni kamati ya Mashindano chini ya mwenyekiti Mohammed Nassor akisaidiwa na wajumbe Makamu Iddi Kajuna na Wajumbe Jerry Yambi, Hussein Simba na Mohammed Omar.
Niwakumbushe tu kuwa mpira wa miguu una njia zake za kuongoza ambazo zinapaswa kufuatwa ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundo mbinu ya ya utawala na usimamizi, katika hili ni pamoja na kutengeneza idara muhimu ndani ya klabu ikiwemo sekretarieti( yaani watendani wa kazi za kila siku) ya klabu ambayo uongozi wenu bado haija waajiri wangine baada ya kuwaondoa kazini aliyekuwa katibu mkuu wenu Ezekiel Kamwaga na msemaji Asha Muhaji.

Umuhimu wa kuwa na kamati mbalimbali ni pamoja na kuwapa nafasi wadau katika maeneo ya usimamizi kwa minajili ya utaalamu wao, kama vile ufundi, fedha, mashindano, sheria mawasiliano na hata kuunda idara mbalimbali ndani ya klabu ambazo zitarahisha utendaji wa kazi na mawasiliano, tofauti na namna mambo yalivyo hivi sasa ambapo maamuzi ya kutimuliwa kazi kwa kocha Logarusic yakiacha maswali mengi katika vichwa vya wapenda soka kote nchini na swali la kama kweli kuna sababu zozote za kiufundi zilitumika kutoa maamuzi hayo magumu.

Kwa maoni yangu nilidhani ingekuwa ni busara kwa viongozi wa Simba kujenga tabia ya uvumilivu kwa yale mambo ambayo mnayaona kwa macho au kuyasikia huku mkifanya tafakari ya kina kabla ya kukimbilia kufanya maamuzi ambayo mwisho wa siku huenda yakaharibu mwenendo mzima wa klabu yenu yenye wanachama na wapenzi wengi nyuma yake.

Iko wazi kuwa wapenzi, wanachama na uongozi wa Simba ulianza kutilia mashaka juu ya uwezo wa Logarusic wakati na baada ya mchezo dhidi ya ZESCO uliofanyika siku ya Simba Day, ambapo Simba ilichapwa bao 3-0, mashaka ambayo hakuna mwenye uwezo wa kuhoji isipokuwa ni yule tu mwenye utaalamu wa kufundisha mpira wa miguu tena mwenye uzoefu na aliyebobea katika taaluma hiyo, vinginevyo nafikiri mmeanza kufanya kazi kwa kusikiliza kelele za watu mitaani.

Mbaya zaidi ni kuwa licha ya kusikiliza kelele hizo, mnafanya maamuzi ya haraka bila kujali athari ya kesho.

Jambo la kusikitisha ni kwamba Simba bado inaendelea na usajili ambao tarehe ya kufunga dirisha itakuwa ni Agosti 17 2014 mujibu wa tangazo la shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF). 

Kocha huyu aliyetimuliwa kazi ndiye aliyekuwa akiongoza benchi la ufundi katika kupendekeza majina na aina ya wachezaji aliokuwa ana wataka kikosini, baadhi ya wachezaji hao wamesha mwaga wino Msimbazi, akiwemo Elias Maguri na Shabani Kisiga 'Malon' swali ni kwamba hivi kweli kocha atakaye kuja atafurahishwa na usajili wa Logarusic ambaye mlimpamba wakati mnampa mkataba mpya wa mwaka mmoja? 

Kinacho nisikitisha ni kwamba wamenukuliwa wachezaji wa Simba baada ya mchezo dhidi ya ZESCO akiwemo Uhuru Selemani, Masoud Nassoro Cholo na mlinda mlango Hussein Sharif 'Cassilas' wakisema kuwa kikosi chao ni kizuri na kocha wao ni mzuri pia ni mzuri, na kwamba matokeo ya mchezo huo yasitumike kama kigezo cha kuwahukumu wao na kocha wao Logarusic kwani kikosi chao kina wachezaji wengi wapya na miili ya wachezaji bado haija nyambulika vizuri kukabiliana na timu kama ZESCO ambayo wachezaji wake wamekuwa pamoja kwa kipindi kirefu.

Inawezekana nikawa naandika mengi na marefu kuhusu kufukuzwa kwa LOGARUSIC kumbe ukweli juu ywa kufukuzwa kwake ukawa nyuma ya pazi, lakini kwa tafsiri ya haraka, siku moja tu baada ya mchezo wa Siku ya Simba     (SIMBA DAY) majibu yake yanakuja wazi wazi ni kiwango cha chini cha timu dhidi ya Wazambia ZESCO.

Kama uongozi uliamua kumuongezea mkataba bila shaka uliridhika na tabia zake,   za ndani na nje ya uwanja iweje leo ionekana kama tofauti na viongozi walivyo tarajia baada ya matokeo ya 3-0. Kumbuka Simba imewahi kupoteza mara nyingi katika siku ya Simba Day na jibu lake ni wazi kuwa mara zote kikosi kinakuwa bado hakija wiva kimashindano hivyo matokeo ya juzi si kigezo.

MAONI YA ROCKERSPORTS
Uongozi mpya wa Simba chini ya Rais Evance Aveva tengenezeni kwanza miundo mbinu ya kiutendani na kiutawala kabla ya kukimbilia matokeo ya uwanjani.