Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imepitisha usajili wa wachezaji wa klabu za
Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza huku wenye kasoro ndogondogo klabu zao
zikitakiwa kuziondoa ili waweze kupatia leseni za kucheza ligi msimu huu wa
2014/2015.
Kasoro
hizo ni kufikia makubaliano na klabu ambazo wachezaji husika wametoka,
kuwafanyia uhamisho (transfer) na kulipa ada za uhamisho. Kamati vilevile
ilibaini wachezaji wengi hawakufanyiwa uhamisho kama kanuni za ligi hizo
zinavyoelekeza.
Hivyo,
klabu ambazo hazitakuwa zimeondoa kasoro hizo kwa wachezaji wao leseni zao
zitazuiliwa mpaka watakapokuwa wamekamilisha kila kitu. Ni wachezaji wenye
leseni tu ndiyo watakaoruhusiwa kucheza mechi za ligi.
Klabu
za African Lyon, African Sports, Ashanti United, Coastal Union, Kiluvya United,
Majimaji, Mji Mkuu, Polisi Dodoma, Polisi Morogoro, Red Coast na Stand United ziliwawekea
pingamizi wachezaji mbalimbali kwa kutofanyiwa uhamisho.
Kuhusu
Ike Bright Obina wa Nigeria aliyewekewa pingamizi na African Lyon dhidi ya
Coastal Union, Kamati imezitaka klabu hizo kufikia makubaliano, na zikishindwa
mchezaji huyo atabaki African Lyon.
Kamati
vilevile ilijadili malalamiko ya Kocha wa zamani wa Simba, Zdravko Logarusic
dhidi ya klabu hiyo, na kuzipa pande hizo mbili siku 14 kufikia muafaka juu ya
malalamiko hayo, na zikishindwa ndipo zirejee tena mbele ya Kamati.
Logarusic
aliyewakilishwa na mwanasheria wake Dickson Sanga anailalamikia klabu hiyo kwa
kuvunja mkataba kinyume cha taratibu, hivyo kutaka Simba imlipe dola 6,000 kwa
kuvunja mkataba, na pia kulipa dola 50,000 ikiwa ni fidia maalumu ya madhara
yaliyotokana na uvunjwaji huo.
No comments:
Post a Comment