Nyota shupavu wa kandanda Cristiano Ronaldo ameweka historia
kama mwanaspoti wa kwanza duniani kupata wafuasi milioni 100 kupitia ukurusa
wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Face Book.
Ronaldo amefikia idadi hiyo jana Jumanne na kuingia kumbukumbu kama
binadamu wa pili katika historia kufikia idadi hiyo nyuma ya mwanamziki
mashuhuri, Rihanna.
Wanamuziki wenye sifa ulimwenguni, Eminem (milioni 96) na mwanadada Shakira (milioni 90) ndio wanafunga nne bora kwenye orodha hiyo
ya watu wenye ‘wapendwa’ au kwa Kimombo ‘likes’ nyingi zaidi kwenye
kurasa zao za Face Book.
Ronaldo ambaye aliifungia taifa lake Ureno goli la ushindi Jumanne
usiku kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Euro 2016 dhidi ya Denmark amekuwa
mhusika mkuu kwenye mtandao huo tangu kufungua ukurasa wake 2009.
Nyota huyo wa miamba wa Uhispania Real Madrid ametumia ukurasa huo
kupatia mashabiki wake fursa ya maisha ya ukwasi wanaspoti mashuhuri
huishi.
Matangazo yake na picha anazoweka kwenye mtandao huo haswa
akijivinjari na sabuni yake ya roho, Irina Shayk likizoni zimetia fora
sana na kuvutia wengi kupenda ukurasa wake.
“Ni heshima kubwa kwangu kufikia ‘wapendwa’ milioni 100 wa
Facebook. Ni jambo la kushangaza kupanda ngazi hii ya utukufu na
kuwasiliana na mashabiki wangu kote duniani. Wao ndio hunipa motisha na
nawashukuru wote,” Ronaldo alisema kwenye taarifa.
Nyota mwenzake na asimu mkubwa wa Barcelona, Lionel Messi anamfuata miongoni mwa wanaspoti na ‘wapenzi’ milioni 74.
No comments:
Post a Comment