Rais wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzaniua (TFF) Leodegar Tenga amesema kuwa shirikisho lake lina imani kuwa
mazungumzo baina yake na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na michezo
pamoja na Mamlaka ya Mapato yatamaliza tatizo la kushikiliwa kwa akaunti
ya Shirikisho kutokana na malipo ya kodi ya mishahara ya makocha wa
kigeni.
Rais
Tenga alikuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi wa TRA
kushikilia akaunti ya TFF ikiielekeza Benki ya NMB kukata kiasi cha Sh
157,407,968/- ikiwa ni malipo ya Kodi Kadri ya Mapato ya Mfanyakazi (P.A.Y.E) ya makocha Marcio Maximo na wasaidizi wake.
Katika
mzozo huo wa muda mrefu, TFF imekuwa ikijitetea kuwa haiwezi kulipa
kodi hiyo kwa kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ndiyo
mlipaji wa mishahara ya makocha hao, ikiwa ni ahadi ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano, Dk Jakaya Kikwete ya kulipia makocha wa michezo tofauti,
ukiwemo mpira wa miguu.
“Hili
ni suala nyeti ambalo linahitaji kumalizwa kwa mazungumzo baina ya
pande zote,” alisema Tenga na kuongeza: “Ninataka kuwahakikishia kuwa
suala hili linazungumzwa na tayari nimeshafanya mazungumzo na maofisa wa
Wizara na tumekubaliana kukutana na pande zote wakati wowote iwe leo jioni au kesho.
“Ni
matumaini yangu kuwa suala hili litakwisha na jana nimetoka Kampala
(Uganda kwenye Kombe la Chalenji) moja kwa moja na kwenda kuzungumza na
viongozi wa Wizara na wamekubali kwamba tuongee pande zote kulimaliza
suala hili.
“Nimezungumza
na wenzetu wa serikali kwa sababu najua unyeti wa suala hili. Pesa
zilizokamatwa si zetu; ni pesa za klabu na zimetolewa na mdhamini ambaye
tumakubaliana namna ya kuzitumia. Fedha hizi hazikutolewa kwa ajili ya
kulipia kodi. Lakini TRA wanazishikilia kwa sababu Premier League iko
chini ya TFF.”
Tenga
alisema kuwa TRA wanafanya kazi kwa kufuata sheria zao za ukataji kodi
na hivyo wana haki ya kufuatilia kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, muajiri
ndiye anayetakiwa kukata kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi.
“Hivyo
hatuwezi kuilaumu TRA kwa sababu ndivyo sheria inavyosema, lakini pia
hatuna uwezo huo wa kulipa fedha hizo kwa sababu, kwanza hatuna na pili
sio sisi tunaolipa mishahara ya hawa makocha,” alisema Tenga.
Akizungumzia
historia ya suala hilo, Tenga aliishukuru serikali kwa msaada ambao
imekuwa ikiutoa katika mpira na kwamba ahadi ya Rais Kikwete ya kusaidia
kulipa makocha wa timu za taifa imeusogeza mpira wa miguu karibu na
serikali na karibu na rais.
“Rais
Kikwete alisema wakati alipoingia madarakani (mwaka 2005) kuwa anajua
kuwa kuna tatizo kwenye mpira na akatoa ahadi ya kulipa walimu wa mpira.
Ahadi hiyo imefanya ukaribu uliopo sasa kati ya mpira na serikali; kati
ya mpira na rais sasa kuwa mkubwa. Serikali imechangia kwa kiasi
kikubwa kwenye mpira, yaani kulipa walimu,” alisema Tenga.
“Sasa
sisi ni administrators wa hawa walimu. Tunachofanya ni kuandaa mikataba
ambayo ni standard duniani kote kwa mujibu wa taratibu za FIFA
(Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu). Kwa kawaida
makocha wa kigeni huwa wanatayarishiwa mikataba ambayo ni tax free
(isiyo na kodi). Baada ya kuingia nao mikataba, huwa tunaipeleka
wizarani ambao ndio wanawalipa makocha moja kwa moja kwenye akaunti
zao.”
Katika
mkutano huo na waandishi, Rais Tenga pia aliipongeza timu ya taifa ya
Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kwa kuanza vizuri mashindano ya Kombe
la Chalenji, akisema ushindi huo ni ishara nzuri hasa kutokana na ukweli
kuwa kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi na akataka
Watanzania waendelee kuiunga mkono.
Tenga
pia alisema kumekuwepo na malalamiko kuhusu makato ya mechi na kwamba
suala hilo ni la muda mrefu na kwamba TFF imepiga hatua kubwa tangu
ilipoanza kulishughulikia.
No comments:
Post a Comment