Kocha
wa timu ya taifa ya vijana, Jacob Michelsen amesema kuwa anajivunia
vijana wake licha ya kuondolewa na Congo kwenye mashindano ya kuwania
nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na kulaumu uamuzi kuwa
ulichangia kwa kiasi kikubwa Serengeti Boys kulala kwa mabao 2-0 mjini
Brazaville.
Kwa
matokeo hayo, Serengeti Boys imeondolewa kwenye mashindano ya Afrika
kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17 kwa jumla ya mabao 2-1 baada
ya mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Dar es salaam kuisha kwa Tanzania
kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa. Timu hiyo
itarejea nchini siku ya Jumanne saa 1:00 jioni kwa ndege ya Kenya
Airways.
“Vijana
walicheza vizuri sana na walicheza kwa juhudi wakati wote wa mchezo na
safari hii wacheza dhidi ya vijana ambao ni wakubwa zaidi,” alisema
kocha huyo kutoka Denmark.
“Lakini waliangushwa na uamuzi kwa sababu
walipata penati ambayo haikustahili".
“Kwa
kweli hata tukio lenyewe lilitokea nje ya penati na beki wetu alilala
kuchukua mpira na alifanikiwa kuufikia bila ya kumgusa mshambuliaji wa
Congo. Lakini wakati beki wetu akiwa ameshauchukua mpira na yule
aliyejiangusha akiwa ameshanyanyuka, mwamuzi alipiga filimbi kuamuru
penati.”
Kocha
huyo alisema pamoja na bao hilo Serengeti Boys iliendelea kucheza
vizuri na nusura mchezo huo uamuliwe kwa penati tano, lakini wenyeji
wakapata bao la pili lililoinyima Tanzania nafasi ya kufuzu kwa mara ya
kwanza kucheza fainali hizo.
“Lilikuwa
ni bao lilitokana na shambulizi la kushtukiza na walikimbia vizuri na
mpira na baadaye kupiga krosi iliyounganishwa kwa kichwa,” alisema
Michelsen.
“Najivunia
vijana wangu kwa sababu walicheza kwa kujituma na kujiamini; walifanya
juhudi kubwa, lakini uamuzi ulituangusha. Nina imani na timu hii na
natumaini kama vijana watano walitoka kwenye timu ya U-20 na kuingia
timu ya taifa, basi kuna vijana wengine wanaoweza kutoka kwenye timu hii
na kuingia timu ya taifa. Ni vizuri tukaendelea na programu za vijana
tuweze kujenga timu nzuri baadaye.”
Afisa
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi ambaye
aliambatana na timu hiyo Congo, alisema mechi hiyo ilizingirwa na
mizengwe kabla na baada ya mechi na kwamba wamesharipoti matukio yote
kwa kamisaa wa mechi hiyo baada ya kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo,
mtunza vifaa Juma Kizwezwe na mkalimani wa timu kushambuliwa na polisi
na mashabiki kabla ya mechi hiyo.
“Hatukupewa
gari la polisi wakati wa kwenda uwanjani na hivyo hatukujua tuingilie
wapi. Tulipofika uwanjani, walituelekeza mlango ambao tuliona
wanaumwagia maji ambayo Julio aliona yangeathiri wachezaji na kuwaagiza
wasitumie mlango huo na ndipo polisi walipomvamia,” alisema Madadi.
“Kizwezwe
alishambuliwa na mashabiki baada ya kamisaa kumuagiza arejee hotelini
kufuata jezi zaidi kutokana na Congo kuwasilisha pingamizi kabla ya
mechi kuwa jezi za Tanzania hazikuwa kwenye mlolongo uliokuwa kwenye
orodha iliyowasilishwa.
“Alipotaka
kutoka uwanjani, alizuiwa na askari na tukalazimika kumuita kamisaa
ambaye aliagiza polisi wamruhusu atoke uwanjani. Alipotoka mashabiki
walimzuia asiondoke na mzozo ulipokuwa mkubwa mashabiki walimvamia na
ndipo tulipomwita tena kamisaa ambaye aliagiza Kizwezwe asiondoke na
badala yake jezi zilizokuwa na matatizo zibandikwe plasta. Hata hivyo,
polisi walimzuia Kizwezwe asiende kukaa kwenye benchi hadi mchezo
ulipoisha.”
Madadi
alisema kuwa kutokana na vurugu hizo, kamisaa huyo kutoka Afrika Kusini
aliomba majina ya walioshambuliwa na akaahidi kuyaweka matukio hayo
kwenye ripoti yake.
Katibu
Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema Shirikisho limeyapokea matokeo hayo
kwa masikitiko kutokana na ukweli kwamba TFF ilifanya juhudi kubwa
katika kuhakikisha safari hii timu za vijana zinapata maandalizi mazuri
na ya muda mrefu, lakini juhudi hizo zimekwamishwa na mazingira mabaya
kama yalivyoripotiwa na viongozi wa msafara wetu.
“Katika
kutafuta mafanikio hakuna njia ya mkato. Ni lazima tuamini katika
program tunazozitekeleza na kuboresha pale tunapoona pana udhaifu.
Tunaamini kuwa itafika wakati juhudi hizi zitazaa matunda na Watanzania
watanufaika na mipango hii ya muda mrefu,” alisema katibu huyo.
No comments:
Post a Comment