Sergio Ramos aliifungia Madrid goli la pili lakini halikutosha kuwabandua nje Borussia Dortmund |
Borussia Dortmund imefuzu katika fainali ya kombe la klabu bingwa Ulaya
kwa mara ya pili katika historia yao, licha ya kushindwa na Real Madrid
mabao mawili kwa sifuri katika mchuano wa mkondo wa pili wa nusu fainali
Dortmund waliishinda Madrid kwa jumla ya magoli manne kwa matatu, baada
ya ushindi wao wa magoli manne kwa moja katika mechi ya mkondo wa
kwanza. Huku wakiitaji muujiza mkubwa wa kubadilisha mambo baada ya
kichapo cha wiki iliyopita, Real walionekana kuishiwa kasi, baada ya
Gonzlo Higuain, Cristiano Ronaldo na Mesut Ozl kupoteza nafasi za wazi
katika dakika za mapema.
Hata hivyo, baada ya Robert Lewandowski kusukuma kombora safi
lililogonga chuma naye kipa Diego Lopez kufanya muujiza na kulizuia
kombora la karibu la Ilkay Gundogan, Madrid walipata nguvu tena katika
dakika ya 83 wakati nguvu mpya Karim Benzema kubusu nyavu kutoka pasi
safi iliyoandaliwa na Ozil.
Na dakika sita baadaye wakapata matumaini ya kweli ya kubadilisha
matokeo hayo baada ya nahodha Sergio Ramos kusukuma bazuka ndani ya
nyavu na kufanya mambo kuwa mawili bila jawabu, ila walihitaji bao la
tatu ili kufuzu.
Dortmund walistahimili dakika tano za kijasho ili kujikatia tikiti ya
kucheza katika fainali itakayoandaliwa kwenye uwanja wa Wembley jijini
London mwezi ujao. Kocha wa Dortmund Jurgen Klopp amesema Real huenda
walikuwa timu bora ya usiku, lakini hilo halikuwa na maana yoyote kwa
sababu vijana wake wametimiza lengo lao la kufika fainali na kwamba
amejivunia mchezo wao. Mwenzake wa Real Jose Mourinho, matokeo hayo
yalimaanisha kuondolewa nje ya dimba hilo katika awamu hiyo kwa mwaka wa
tatu mfululizo.
Dortmund sasa ni miamba Ulaya
Klopp amesema kuwa sasa Dortmund wanapaswa kutambulika kama
mojawapo ya timu mahiri za soka barani Ulaya baada ya kuwabandua nje
Real Madrid. Ameongeza kuwa hawajali ni nani watakayekutana naye katika
fainali, lakini kila mtu ataona kuwa hawatakwenda Wembley kama watalii
bali kushinda kombe.
Klopp hata hivyo amemshutumu refarii Muingereza Howard Webb akisema kuna
matukio ambayo beki wa Madrid Sergio Ramos alistahili kupewa adhabu
kali, kutokana na namna alivyokuwa akimchezea kimabavu Robert
Lewandowski.
Wakati Klopp akilalamika kuhusu Ramos, naye Mourinho anadai kuwa
refariii alistahili kumtimua uwanjani Mats Hummels kwa kuunawa mpira
katika kipindi cha pili. Matokeo hayo ya Real Madrid yameendelea kuibua
maswali kuhusiana na hatima ya Mreno huyo. Mourinho amesema atasubiri
hadi mwisho wa msimu ili kujadili na wasimamizi wa klabu kuhusu mkataba
wake.
Mourinho amesema anafahamu kuwa anapendwa nchni England, anapendwa na
mashabiki na vyombo vya habari. Anasema “ninapendwa na baadhi ya vilabu,
hasa kimoja. Lakini Uhispania mambo ni tofauti, watu kadhaa
wananichukia, wengi weu ndani ya chumba hiki”.
Katika mechi ya pili leo, Barcelona wanawakaribisha Bayern Munich ambao
wakilenga kugeuza matokeo ya mkondo wa kwanza ya mabao manne kwa sifuri.
Barcelona watastahili kufanya kazi ya ziada uwanjani Camp Nou katika
kuzuia kile wengi wanaona kitakuwa ni Fainali ya timu mbili za Ujerumani
uwanjani Wembley, “Der Klassiker”.
Mwandishi: Bruce Amani/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman
No comments:
Post a Comment