Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiomba Serikali, taasisi na kampuni
mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake kwa
vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda kwa mechi ya Kombe la
Dunia dhidi ya Msumbiji.
Timu
hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani Pwani chini ya Kocha
Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza
itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya TFF, Lina Kessy amesema hiki
ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri
katika mashindano hayo.
Ameitaka
jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo haina mdhamini wala
mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya kusubiri ifanye
vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.
Kessy
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake
Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa fursa ya kambi
kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia huduma nyingine
inazopata hapo.
Vilevile
amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutokana na
ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira wa miguu wa wanawake
kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.
“Shukrani
za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao wachezee timu ya Taifa, kwani
wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa wazazi. Pia
tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia
wachezaji wetu,” amesema.
Fainali
za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo
Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza
na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe.
No comments:
Post a Comment