"Hivi karibuni niliteuliwa na Mwenyekiti wa Klabu ya
Simba Mhe Ismail Aden Rage kuwa mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya Simba.Wanachama na wapenzi wengi wa Simba kutoka
sehemu mbali nje na ndani ya nchi
walinipiga simu, wengine wakinitaka nikatee uteuzi na wengine wakinitaka
nikubali uteuzi, kila mmoja akiwa na
sababu zake, Wakati napokea uteuzi huu
na kutafakari ilibidi nijiridhishe
katika mambo mbalimbali yakiwemo
yafuatayo:
1. Uhalali wa uteuzi huu kisheria na hasa
kwa kuzingatia hali halisi ya
sasa ya siasa za Klabu.
2. Nini mantiki ya
kuteuliwa kwangu wakati huu wa
mgogoro na nini hasa nafasi yangu.
3. Nini utakuwa mchango wangu katika kamati ya Utendaji
katika wakati huu na baadaye.
4. Wajibu wangu ni nini kama mwanachama wa Simba.
5. Nini chanzo cha mgogoro huu wa Simba na ulazima wa
wanachama wa Simba Kuingia Katika Mgogoro huu.
6. Utayari wa pande mbili zinazopingana kurudi katika meza
ya Mazungumzo
7. Athari za muda mfupi na Mrefu kwa Klabu ya Simba kwa kurejea migogoro mbali mbali iliyo
wahi kutokea katika siku za Nyuma.
8. Kina nani hasa watakaofaidika zaidi na mgogoro huu
(viongozi wa Simba, Wanachama wa Simba, Klabu ya Simba au wapinzani na maadui wa Simba).
9. Nini Nafasi ya TFF katika kutatua na Kupatia ufumbuzi wa
mgogoro huu.
Baada ya kujiuliza na kutafakari nilitambua na kujiridhisha
kama ifuatavyo:
1. MAMALAKA YA MWENYEKITI KUTEUA WAJUMBE WAWILI WA KAMATI YA
UTENDAJI YA SIMBA
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba Ibara ya 28(1)(d) mwenyekiti
anaweza kuteua wajumbe wawili kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya Simba , bila
kutoa nafasi ya Wateuliwa kuuliza
wameteuliwa kutoka katika kundi lipi kati ya Wajumbe wawili. Kwa mantiki hiyo
mwenyekiti anapewa nguvu za kikatiba
kuteua wajumbe wawili ambao anaona wanaweza kumsaidia katika shughuli mbalimbali za kuendesha klabu na sio zawadi
au shukurani kama ambavyo wengi wamekuwa wakitafsiri,nadhani jambo muhimu la
kuhoji ni wanaoteuliwa wanakwenda kufanya nini kwenye kamati ya Utendaji kwa
maana ya uwezo wao kuisaidia Simba na sio nani ateuliwe na nani asiteuliwe
kwani hilo liko katika mamalaka ya
mteuzi alimradi tu anayeteuliwa ni mwanachma wa Simba na ataongeza tija
kwa klabu.
2. NINI MANTIKI YA KUTEULIWA
KWANGU KATIKA WAKATI HUU WA
MGOGORO NA NINI HASA NAFASI YANGU
Wanachama na wapenzi wengi wa Simba walitafsiri uteuzi huu
umefanyika kwa nia ya kumsaidia mwenyekiti ili aendelee kukaa madarakani, watu
wenye mawazo hayo pamaoja na wengine waliokuwa na mawazo tofauti na hayo hawakuangalia na kuzingatia kwa upana sababu za uteuzi huu, Ukweli ni
kwamba wajumbe wote wa kamati ya Utendaji ya Simba akiwemo mwenyekiti walikuwa
ni sehemu ya mgogoro huu hivyo isingekuwa rahisi pande zinazopingana kutafuta suluhu kama itahitajika, hivyo ni
wazi ni mtu mwingine mwenye uzoefu
na uwezo wa kutatua mgogoro huu na ambaye hakuwa na upande wowote katika mgogoro
huo alihitajika , aidha ninamini kuwa
Uzoefu wangu katika uongozi wa mpira wa miguu na Elimu yangu Ulifaa
kuingia katika Kamati ya Utendaji ya Simba ili pamoja na mambo mengine
niweze kutafuta na kurejusha amani katika Simba , ninapenda ieleweke kuwa
katika mgogoro huu mimi sikuwa na sina pande wowote katika pande mbili zinazopingana , jambo lililonifanya kujiuliza ikiwa nitakubali uteuzi huu Simba Itafaidika na nini na kama
nikikataa uteuzi Smba itapata hasara
kiasi gani, niligundua kukataa kuna athari kubwa zaidi kwa Simba aidha ingekua
pia ni udhaifu na kukosa ukomavu katika uongozi ambao kwa kiasi kikubwa uamuzi
huo ungetafsiriwa ni kuweka mbele ubinafsi badala ya maslahi ya walio wengi na
klabu, watu wengi walijiuliza inakuwaje Rage
kumteua Wambura na mimi kukubali
kufanya kazi nae hasa ukizingatia
mahusiano yao katika siku za nyuma katika utawala wa mpira wa miguu, Jibu langu
ni kuwa SIMBA KWANZA MAHUSIANO YA MTU NA
MTU BAADAYE.
3. NINI UTAKUWA MCHANGO WANGU WA SASA NA SIKU ZA
BAADAYE KWA SIMBA.
Baada ya kutafakari kwa
kina mchango wangu kama mjumbe wa kamati ya Utendaji ya Simba kwa siku
za usoni, niligundua ya kuwa sitakuwa na msaada wowote kwa klabu yangu kama
mgogoro huu hautakwisha na viongozi kurudi katika meza moja na kufanya kazi
ambayo wanachama wa Simba walitegemea wafanye wakati wanawachagua, hivyo niliona ni vyema nikachukua jukumu la
kuingilia kati mgogoro huu ili niweze
kujua nini hasa kiini cha mgogoro huu katika Uongozi wa Simba. Nilipata
nafasi ya kuongea na Mwenyekiti wa Simba na
kisha kuongea na mjumbe mmoja moja waliochaguliwa wa Kamati ya Utendaji na Kisha kukutana nao
kwa pamoja katika siku tofauti tofauti, ili kujua kiini na sababu za
sintofahamu iliyokuwa inaendelea ndani ya Uongozi wa Simba, Kwanza nina penda
kuwashukuru wajumbe wote wa kamati ya
Utendaji ya Simba Kwa Ushirikano mkubwa na mzuri walionipa, ufahamu wao na uelewa wao wa masuala ya Simba umeonyesha ukomavu mkubwa na weledi katika uongozi wa Simba, tumefanya mazungumzo
marefu , makubwa na ya Kina juu ya mstakabali wa Klabu yetu, wajumbe walikuwa na masikitiko na
manung’uniko mbalimbali ya msingi ambayo kimsingi mwenyekiti atakaporejea atakutana
na kamati yake ili mamabo ya msingi yaliyozungumzwa yafanyiwe kazi na kupanga
utekelezaji wake. Mwenyekiti ameisha
taarifiwa juu ya auamuzi huu. Msingi wa
mazungumzo yetu uliegemea zaidi athari ambazo Klabu yetu ingeezipata katika
kipindi hiki kuelekea ligi Mzunguko wa pili na mchezo kati yetu na Mahasimu
wetu YANGA katikati ya mwezi wa December pamoja na athari
nyingine ambazo klabu yetu ingepata kimapato kupitia wadhamini na wafadhili mbali mbali walio na mikata na
wasio nayo, aidha wapenzi na wanachama wengi wasiopenda migogoro wameamu kukaa mbali na Timu yetu viwanjani na
nje ya uwanja, aidha wapenzi wengi wa Simba wamepoteza ujasiri wa kuizungumzia
na kuitetea Klabu yao mitaani popote walipo kwa kuwa hawajui siku inayofuata
kutatokea jambo gani litakalo
wakarahisha, kwa kuzingatia hayo yote ndio maana wajumbe wakaridhia mazungumzo
ya kutafuta amani na umoja katika klabu yaendelee na sasa anasubiriwa
mwenyekiti ili nae atumie busara zake kumaliza mvutano huu ambao kwa sasa
umeisha fikia tamati kati ya 85%-90%.
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba Ibara 28(1)MUUNDO WA KAMATI YA
UTENDAJI “Kamati ya Utendaji inaundwa na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na
wajumbe waliochaguliwa na Mkutano Mkuu
pamaoja na wajumbe walioteuliwa”aidha ibara hiyo inasomeka pamoja na ibara ya
33(1)&33(3)a,b,c,d,e,f,g,h. Kwa mantiki hiyo bila Mwenyekiti hakuna Kamati
ya Utendaji na Mwenyekiti bila wajumbe hakuna Kamati ya utendaji jambo ambalo
lingepelekea Simba kusimsmisha shughuli zote kwani shughuli zote za Simba
muhimu zitafanyawa na kuidhinishwa na kamati ya Utendaji kwa mujibu wa katiba
ya Simba ibara ya 30(1)a,b,c,d,e,f,g,h,i,j,k,l,m.
Aidha katika kuendeleza nia ya kuifanya Simba Moja
nitajitahidi katika siku za hivi karibuni nikitane na wanachama wa Matawi ambayo yanaonekana au kuhisiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na uongozi wa
Simba kama (Mpira Pesa, Vuvuzela na mengine) ili kujua sababu za kutokuwa na
mahusiano Mazuri na uongozi ili kutafuta suluhisho la kudumu na hatimae washirki
katika shughuli za klabu na kuifanya Simba
Moja isiyokuwa na wanachama wenye matabaka kwa sabau yoyote ile.
4. NINI WAJIBU WANGU KAMA MWANACHAMA WA SIMBA
Wajibu wangu wa uwanachama kama walivyo wanachama
wengine ni wa hiari kwani kila mmoja
wetu alichagua kuipenda Simba kwa hiari yake bila Shuruti lolote na bila kujali
atapata nini kibinafsi aidha kimaslahi au kiuongozi zaidi ya furaha na
maendeleo ya Simba, hivyo kila
mwanachama anawajibu kikatiba na kikanuni kuilinda , kuitumikia na kuiteteta
klabu ili ifikie malengo bila kuvunja taratibu na misingi tuliojiwekea,
inasikitisha kuona siku hizi kuna baadhi ya watu wako hiari kuona na
kusababisha timu ifungwe eti tu kwa kuwa hampendi kiongozi Fulani aliyeko
madarakani, hiyo haikubaliki na ninawaomba wanachama na wapenzi wa Simba ikiwa
watambaini mtu wa aina hiyo Katika klabu yetu ashughulikiwe mara moja , kwani
kuna watanzania wengi na wapenzi mbali
mbali wa Simba nje na ndani ya
Dar-es-salaam(MARA , MTWARA,MANYARA, SONGEA nk) ambao hawajui nini
kinachoendelea hapa ila wanaumia sana timu inapofanya vibaya katika michezo
mbalimbali. Kuhujumu klabu sio tu kwa kufungisha timu bali hatu kununua na
kuuza vifaa bandia vya michezo
vinavyojitambulisha na klabu huku ukijua wazi
klabu haipati mapato yoyote wote hawa wanastahili adhabu sawa na stahiki,
kutokana na matukio mbalimbali ya kujaribu kuondoa viongozi kabla ya muda wao
wa uongozi kuisha na bila mafanikio inapashwa
kuwa somo tosha kwa wanachama kuwa makini wakati wa uchaguzi kuchagua viongozi
wanaowafahamu uwezo wao bila kurubuniwa kwa zawadi na pesa ndogo ndogo, kwani
katika mfumo wa dunia ya leo sio tu kwenye Siasa hata katika mpira kuanzi
FIFA,CAF,TFF mapinduzi yamefutwa na hayakubaliki tena kwa sababu yoyote ambayo
iko nje ya utaratibu wa kikatiba.
Mwanachama unamchagua
kiongozi awe madarakani kwa miaka 4 ambayo ni sawa na siku 1460, ukifanikiwa
kuuza kura yako kwa Shs 50,000 wakati wa uchaguzi ni sawa na kuuza na kulipwa shilling 34.24 kwa siku ambayo haikutoshi hata nauli ya kuja mjini
huko ni kuhujumu klabu kama wengine,
nawaomba wanachama wenzangu tuamke tutoke kwenye usingizi huo usioleta tija
wala maendeleo na mwisho ni migogoro isiyokwisha katika klabu.
5. NINI CHANZO CHA MGOGORO HUU WA SIMBA NA ULAZIMA WA WANACHAMA WA SIMBA KUINGIA KATIKA MGOGORO HUU.
Baada ya kuongea na
pande zote mbili katika mgogoro huu nimebaini sababu kubwa za mgogoro ni:
(i) Mawasiliano(communication) hafifu ndani ya kamati ya
utendaji jambo linalosababisha baadhi ya wajumbe kutokujua baadhi ya mambo
(ii) Kukosekana kwa
Dira na mwelekeo (Vision) jambo linalofanya kamati ya utendaji wote au
mmoja mmoja kukosa mwongozo wa kujua wapi klabu inaelekea.
(iii) Kukosekana kwa uamuzi wa pamoja na uwazi (collective
Decissions and Transparence) katika
baadhi ya mambo katika uendeshaji wa
klabu.
(iv) Kukosa kuaminiana (Trust) miongoni mwa wajumbe wa
kamati ya utendaji
(v) Kukosekana kwa Kanuni (regulations) mbalimbali za uongozi
na Utawala, usimamizi wa Fedha, nk.
(vi) Kukosekana kwa mafuzo, warsha , semina na kozi mbali
mbali za utawala kwa kamati ya utendaji ili kila mmoja ajue wajibu na mipaka ya
madaraka yake katika Klabu.
Baada ya kubaini
mapungufu hayo, niliona hizi ni
kasoro ambazo zinaweza kurekebishika ndani ya kamati ya utendaji yenyewe ikiwa
pande zote zinaweza kukiri mapungufu haya na kutenga wasaa na rasilimali ili
kuondoa kasoro hizo.
Kuhusu wanachama kuingilia mgogoro huu nina amini wanachama
wana nafasi yao katika kuleta na kutatua migogoro mbalimbali, lakini katika
mgogoro huu wa sasa ulikuwa kati ya mwenyekiti na Wajumbe wake wa Kamati ya
Utendaji, hivyo ilikuwa mapema mno kwa wanachama kuingilia mgogoro huu kwa
sababu bado ulikuwa ndani ya uwezo wa kamati ya utendaji ya Utendaji ya Simba.
6. UTAYARI WA PANDE MBILI ZINAZOPINGANA KURUDI KATIKA MEZA
YA MAZUNGUMZO
Baada yakuwasiliana na kukutana na pande zote mbili za
mgogoro huu, ninapenda kuzishukuru kwa kukubali kukutana ili kumaliza tofauti
zao, ni wazi kwenye usuluhishi ni lazima pande zote zitapata na kupoteza kiasi
cha matarajio yake sio rahisi upande mmoja ukapata ilichohitaji yenyewe kwa
100% hivyo ni wazi pande zote kwa
kuzingatia umuhimu wa mapatano kwa mustakabali wa Simba Watakaa na kukubaliana
kuondoa tofauti zao na kisha kila pande utafuata na kuheshimu katiba na kanuni kama muongozo katika
kufanikisha malengo ya Simba, mwisho wa usuluhishi hakuna upande utakao kuwa
umeshinda au kushindwa isipokua Simba
ndio itashinda, ni imani yangu watatambua nje ya Simba hakuna
aliyemaarufu miongoni mwao, na pia nana penda kuwashauri wapambe wa pande zote
kujiepusha na kutoa maneno ya kuudhi na
kejeli kwa upande mwingine ili kujenga umoja katika Simba.
7. ATHARI ZA MUDA MFUPI NA MREFU KWA KLABU YA SIMBA KWA KUREJEA MIGOGORO MBALI MBALI ILIYO
WAHI KUTOKE KATIKA SIKU ZA NYUMA.
Mgogoro wowote una matokeo Chanya au Hasi (+ve or –ve
results) wakati mwingine migogoro imesaidia kuwakumbusha watawala umuhimu wa
kuwatawala watawaliwa kama walivyo
kubaliana kupitia Katiba lakini wakati mwingi migogoro inaishia kuboma kama
ilivyo kuwa kwa Yanga kuzaliwa Pan Africa na kwa Simba Kuzaliwa Red Star, hivyo
ni jukumu la wahusika kupima kabla ya kuingia katika mgogoro juu ya matokeo
yake ya mwisho, kumbukumbu zangu zinanionsha hakuna kiongozi aliyewahi kupita
Simba bila migogoro kutokea na hakuna hata mgogoro mmoja uliowahi kuleta
matokeo chanya zaidi ya kurudisha nyuma maendeleo ya simba, baadhi ya migogoro
ilipelekea hadi baadhi ya viongozi
kupoteza maisha(marehemu Mzee Juma Salum na mhasibu wa Simba) wakiwa safarini wakijaribu kumaliza mgogoro,
baadhi ya viongozi wa Simba waliokutana na
migogoro ni pamoja na Mzee Hassan
Brashi,Marehemu Ngonya, Marehemu mzee
Bamchawi,Mzee Hazali,Mzee Chamshama, Mzee Dalali na wengine wengi ambapo
migogoro yote hiyo haikuisaidia wala
kuleta tija kwa Simba, kuna wakati Simba ilikaa karibu ya miaka mitatu bila ya kuwa na uongozi wa
kuchaguliwa Kisheria. Hivyo ni wajubu wa wana Simba tupime na tuamue kama
mgogoro huu una tija hasa ukizingatia muda wa uongozi huu inaishia mwezi wa
5(may) 2014 na uchaguzi kufanyika, rai yangu kwa wanasimba kufikiria, kumpima
na kutafakari ni kiongozi gani tuna muhitaji kutaongoza kwa miaka 4 ijayo
kuanzia 2014 badala ya kusinzia na kuamka wakati wa uchaguzi na kuchagua mtu
asiye sahihi na baada kujaribu kumng’oa
kwa kupitia mlango wa nyuma, “mke mzuri hupewa na mwenyezi Mungu ila kiongozi
mbovu humchagua wewe mwenyewe na mungu hukubariki ukae nae kwani umemchagua mwenyewe
kwa hiari yako”.
8. KINA NANI HASA WATAKAOFAIDIKA ZAIDI NA MGOGORO HUU
(VIONGOZI WA SIMBA, WANACHAMA WA SIMBA, KLABU YA SIMBA AU WAPINZANI WA SIMBA)
Kimsingi wanaoipenda na kuitakia mema Simba hawawezi kwa
njia moja au nyingine kufurahia migogoro ya Simba kwani inatia maudhi na
kukatisha tamaa ninaamini hata wanachama wengi binafsi hawapendi hali hii, ila kuna baadhi ya watu wachache
hawasemi ila wanafaidika binafsi
kimapato na hali ilivyo sasa na wakati mwingine wa migogoro, viongozi wa
Simba hawana faida na migogoro hii kwani inawafanya washindwe kufanya kazi
waliyowaahidi wapiga kura wao wakti wa uchaguzi.
Wanaofaidika kwa kiwango kikubwa na mgogogro wetu ni
mahasimu na wapinzani wetu kwani wana
hakika bila umoja, mshikamano na upendo hatuwezi kuwa na timu ya Ushindani,
hivi sasa timu yetu iko nafasi ya 4 mgogoro huu ukiendelea unaweza kutupeleka
pabaya zaidi hata kufika kushuka daraja, wanaokumbuka historia ya Simba wakati wa Marehemu J.D.Ngonya, tuliwahi
kuponea kushuka daraja mechi ya mwisho ya ligi sababu ya migogoro, na wakati ule
upinzani haukuwa mkali kiuchumi na kimiundombinu ya mpira kama wakati huu, hivyo wana Simba tusitumiwe na kutumia mikono
yetu wenyewe kuivunja klabu yetu, tupambane na adui wa nje halafu ndio
tuulizane wenyewe tukiwa ndani hakuna haja ya kuchochewa na maadui zetu na
kisha
kuyatangaza matatizo
yetu hadharini halafu tunaona ujiko, sifa na ufahari, hii ni hatari kwa Klabu
hasa katika biashara kwa maana ya uwekezaji na udhamini kwani hakuna mfanyabiashara anayependa kuwekeza
mahali kwenye fujo na kusiko na utulivu.
9. NAFASI YA TFF KATIKA KUTATUA NA KUPATIA UFUMBUZI WA
MGOGORO HUU.
Simba ni mwanachama wa TFF ambapo TFF ni mwanachama wa FIFA,
kimsingi chombo kikuu kinachosimamia
Mpira wa Miguu hapa nchini ni TFF hivyo katika mfumo wa uongozi na uendeshaji
wa mpira duniani kila nchi ina chombo kinacho tambuliwa na FIFA katika
kusimamia mpira wa miguu katika nchi mwanachama hivyo kwa Tanzania ni TFF , kwa mantiki hiyo kupingana na TFF
kunaweza kuleta hatari na madhara makubwa zaidi kwa Simba, kwani TFF haiwezi
kuifutia Simba usajili wake ila inaweza kuisimamisha au kuifukuza
uanachama pale inapoona inapingana na
maamuzi yake, mfano ulitokea kwa
Tanzania kufungiwa na FIFA 2000 baada ya kukataa maagizo ya FIFA japo wakati
huo FAT ilikuwa na katiba yake, mwaka 2004 Fifa ilifupisha kipindi cha uongozi
wa FAT kutoka miaka 4 hadi 3 kwani uchaguzi ulikuwa ufanyike 2005 kama katiba
ya FAT/TFF ilivyo kuwa inaelekeza, hivyo sio busara kwa Simba ambaye ni
mwanachama wa TFF kupingana nayo,Katiba ya Simba Ibara ya 11(1)f inazungumzia Wajibu wa Mwanachama “Asiwe na
uhusiano wowote wa kimichezo na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa” na hata
katiba ya TFF inacho kifungu hicho hivyo Simba inaweza
kujikuta katika kisiwa ikiwa itatengwa na TFF. Kwa kuwa suluhisho linaelekea
kupatika ni matarajio yangu kuishirikisha TFF katika kufikia makubaliano na
kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya suluhu . Ni matumaini yangu wahusika
watanielewa kwani huu ni mtazamo wangu binafsi bila kushauriwa na upande wowote
na ambao hauna lengo la kuusaidia upande
wowote wa mgogogoro huu zaidi ya kuzingatia maslahi na mustakabali wa Simba
Sports Club kwa Sasa na kwa siku zijazo, ni matumaini yangu Viongozi na
Wanachama wa Simba watachukulia maoni haya kama changamoto na sio vinginevyo,
na kwa wale ambao wengependa kuhukumu basi vyema kwanza kuzingatia yafuatayo
i): Laws(sheria zilizopo),ii) Evidence(Ushahidi uliopo) na Iii) Facts of the matter(Uhalisia wa
jambo).
MUNGU IBARIKI SIMBA, MUNGU IBARIKI TANZANIA. AHSANTENI
Michael Richard Wambura.
Nakala:
:Mwenyekiti Simba Sports club
:Rais- TFF
No comments:
Post a Comment