Kiungo wa AC Milan, Kevin-Prince Boateng, amejiunga na Schalke 04 kwa
mkataba wa miaka mitatu siku ya Ijumaa (30.08.2013). Anakiri ana furaha
kurejea katika ligi ya Ujerumani, Bundesliga.
Inaripotiwa kwamba Schalke iliwalipa wataliana euro milioni 12 kumpata
Kevin -Prince Boateng, nyota wa timu ya taifa ya kandanda ya Ghana. na
mkataba wake unajumuisha uwezekano wa kuongezewa msimu wa nne.
"Bundesliga ndio ligi nzuri kabisa ulimwengu na ndiko wachezaji bora
duniani wanakokwenda," alisema mchezaji huyo wa umri wa miaka 26 katika
mkutano na waandishi wa habari mjini Gelsenkirchen. "Nimesema kila mara
kwamba nilitaka kucheza nchini Ujerumani."
Kevin, ambaye ni kakake mchezaji wa safu ya ulinzi wa timu ya Bayern
Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Jerome Boateng, alianza kibarua
cha kucheza soka katika klabu ya Hertha Berlin na kuhamia Tottenham
Hotspur, England, kwa kitita cha euro milioni 7.9 mnamo mwaka 2007.
Alirejea kwa muda mfupi Ujerumani kwa mkopo katika timu ya Borussia
Dortmund, mahasimu wa Schalke, kabla kujiunga na Portsmouth na baadaye
kwenda Milan.
Ni mchezaji mahiri
Boateng alifunga mabao mawili katika ushindi wa Milan siku ya Jumatano
dhidi ya PSV Eindhoven katika duru ya pili ya mchuano wa mchujo na
kufaulu kushiriki mashindano ya kuwania kombe la mabingwa wa Ulaya,
Champions League, msimu huu kwa jumla ya magoli 4-1.
"Ni mchezaji wa kipekee mwenye uwezo mkubwa na ujuzi wa uongozi,"
amesema kocha wa Schalke, Jens Keller.
Pamoja na nyota wa Schalke,
Julian Draxler, mwenye umri wa miaka 19, Boateng huenda akaunda
ushirikiano imara. Meneja wa Schalke, Horst Heldt, amefutilia mbali
uwezekano wa kumuuza Draxler kabla muda wa wachezaji kuhamia timu
nyengine kumalizika wiki ijayo.
"Itakuwa hatua ya kuchanganyikiwa kumpa
mkataba mchezaji mzuri kisha baadaye umuache mwingine aondoke. Hilo silo
tunalolitaka," akaongeza kusema Heldt.
Boateng anaweza kucheza katika mechi ya leo dhidi ya Leverkusen, licha
ya kufungiwa mechi nne wakati alipotolewa uwanjani kwa kumpiga usoni
mchezaji wa timu nyingine katika mechi yake ya mwisho kati ya Dortmund
na Wolfsburg mnamo mwaka 2009.
No comments:
Post a Comment