TAIFA STARS KUPIGA KAMBI MBEYA
Kikosi cha Taifa Stars kinatarajia
kuondoka keshokutwa (Julai 24 mwaka huu) kwenda Mbeya ambapo kitapiga kambi ya
wiki moja kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Msumbiji.
Mechi hiyo ya raundi ya pili ya
michuano ya Afrika kutafuta tiketi ya kushiriki Fainali za Afrika (AFCON)
zitakazochezwa mwakani nchini Morocco itafanyika wikiendi ya Agosti 2 na 3
mwaka huu nchini Msumbiji.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager itaondoka nchini Julai 31 mwaka huu kwenda Johannesburg, Afrika
Kusini ambapo itafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kutua Maputo kwa ajili ya
mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa wa Zimpeto.
Tunawashukuru
washabiki wote waliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa kuishangilia Taifa Stars
katika mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
MUDA WA USAJILI WAONGEZWA KWA WIKI MBILI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza muda wa usajili kwa wiki mbili ili
kuzipa klabu nafasi ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa. Hivyo hatua ya kwanza
ya usajili inakamilika Agosti 17 mwaka huu badala ya Agosti 3 ya awali.
Kutokana na
marekebisho hayo, kipindi cha uhamisho kinakamilika Agosti 17 mwaka huu wakati
pingamizi itakuwa kati ya Agosti 19 hadi 26 mwaka huu.
Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji itathibitisha usajili kati ya Septemba 1 na 2
mwaka huu.
Uhamisho wa
kimataifa, usajili wa wachezaji huru, na utatuzi wa dosari za usajili unatakiwa
uwe umekamilika kufikia Septemba 7 mwaka huu. Uthibitisho wa hatua ya mwisho ya
usajili utafanywa Septemba 15 mwaka huu.
Kwa upande
wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2014/2015 itaanza Septemba 20 mwaka huu,
na ratiba itatolewa mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment