Brazil na Ujerumani zimefuzu hatua ya nusu fainali ya kombe la dunia baada ya ushindi wa
magoli 2-1 na 1-0 dhidi ya Colombia na Ufaransa, na sasa miamba hao
wawili watamenyana Jumanne mjini Belo Horizonte, bila Neymar.
Goli la mapema la nahodha wa Brazil Thiago Silva na mkwaju wa adhabu
uliyopigwa na David Luiz kutoka umbali mrefu ilitosha kuwapa ushindi
wenyeji wa mashindano hayo na kuwaondoa Colombia katika kinyang'anyiro
cha wanane bora mjini Fortaleza.
Nyota wa Colombia James Rodriguez aliondoka uwanjani akibubujikwa
machozi, baada ya goli lake la sita la mashindano hayo, ambalo
lilitokana na mkwaju wa penati katika dakika ya 80 kutotosha kuizuwia
Brazil kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali mjini Belo Horizonte
siku ya Jumanne.
NEYMAR
Furaha ya ushindi yakatizwa na kujeruhiwa kwa Neymar
Ushindi wa Brazil uligubikwa na habari za kusitikisha kwa wenyeji,
kufuatia kujeruhiwa kwa nyota wao Neymar ambaye ameelezwa kutoweza
kushiriki michezo iliyobaki. Neymar naye aliondolewa machela katika
dakika za mwisho za mchezo huo baada ya kuumizwa, na daktari wa timu ya
Brazil Rodrigo Lazma aliiambia Televisheni ya Brazil kuwa itamchukua
wiki kadhaa kupona.
Madaktari wamesema amevunjika uti wa mgongo
Neymar ambaye amefunga magoli manne katika mashindano hayo na kuongoza
mashmabulizi ya Brazil, aliumia baada ya makabiliano na Juan Zuniga wa
Colombia katika dakika ya 88 na alionekana kuwa na maumivu makali.
Naye nahodha wa timu hiyo Thiago Silva ataukosa mchezo dhidi ya
Ujerumani baada ya kupewa kadi mbili za njano, na hivyo kusimamishwa.
Ni marudio ya mwaka 2002
Nusu fainali kati ya Brazil na Ujerumani itakumbushia mashindano ya
kombe la dunia ya mwaka 2002 ambayo miamba hao wa Amerika Kusini
walishinda kwa magoli 2-0. Hii itakuwa mara ya pili kwa Ujerumani na
Brazil kukutana katika nusu fainali, lakini wachezaji wa Brazil, kiungo
Hulk na Centre half David Luiz wamesema mechi hiyo ya nusu fainali
wanaichukulia kama fainali.
Olivier Giroud wa Ufaransa akisikitika baada ya timu yake kuondolewa na Ujerumani. |
Ujerumani imeweka rekodi ya kufuzu hatua ya nusu fainali kwa mara ya nne
mfululizo baada ya goli la kichwa la mchezaji wa Borussia Dortmund Mats
Hummels kuwasaidia kuishinda Ufaransa goli 1-0 katika uwanja wa
Maracana mjini Rio de Janeiro.
Hummels ambaye ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, alieleza
kushangazwa na mafanikio waliyoyafikia hadi sasa katika mashindano hayo,
akiongozea kuwa ndoto inakaribia kuwa ya kweli sasa.
Kwa upande wake kocha wa Ujerumani Joachim Löw, amesema timu yake
itakuwa na wakati mgumu katika nusu fainali hiyo kwa kuzingatia kuwa
Brazil itakuwa inachezea nyumbani ambako ina mashabiki wengi.
Michezo ya robo fainali inaendelea jioni ya leo ikizikutanisha Uholanzi na Costa Rica na Ubelgiji itatoana jasho na Argentina.
No comments:
Post a Comment