NDANDA, WARRIORS ZASAKA UONGOZI FDL
Green
Warriors ya Dar es Salaam na Ndanda ya Mtwara zinaumana kesho (Oktoba 9
mwaka huu) katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo mshindi
atakamata uongozi wa kundi A.
Mechi
hiyo ya raundi ya tano itachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam ambapo timu itakayoshinda itafikisha pointi kumi na kuipiku
African Lyon inayoongoza sasa kundi hilo ikiwa na pointi tisa.
Kwa
upande wa kundi B kutakuwa na mechi tatu ambapo Polisi Morogoro
inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi tisa itakuwa ugenini dhidi ya
Majimaji inayokamata mkia ikiwa na pointi moja. Mechi itachezwa Uwanja
wa Majimaji mjini Songea.
Kurugenzi
itakuwa kwenye uwanja wake wa Wambi ulioko Mafinga mkoani Iringa
kuikabili Burkina Faso ya Morogoro wakati Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi
mkoani Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Kimondo na Mkamba
Rangers.
LIGI KUU TANZANIA BARA MGAMBO SHOOTING MAJARIBUNI KWA AZAM VPL
Baada
ya kupoteza mechi mbili nyumbani, Mgambo Shooting iko ugenini kesho
(Oktoba 9 mwaka huu) kuikabili Azam katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom
itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Mgambo
Shooting yenye pointi tano, ikiwa nafasi ya pili kutoka mwisho
imeshinda mechi moja tu dhidi ya Ashanti United huku ikipoteza mbili
nyumbani dhidi ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Kocha Mohamed Kampira
ana kibarua cha kuhakikisha anapata pointi mbele ya Azam.
Mechi
nyingine za ligi hiyo ni Rhino Rangers itacheza na Mbeya City kwenye
Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati JKT Ruvu watakuwa wageni
wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani
Morogoro.
Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa shuhuda
wa mechi kati ya wenyeji Oljoro JKT na Ruvu Shooting ya Pwani
inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa.
UCHAGUZI BODI YA LIGI SASA OKTOBA 25
Uchaguzi wa viongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) sasa utafanyika Oktoba 25 mwaka huu badala ya Oktoba 18 mwaka huu.
Kamati
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesogeza
mbele uchaguzi huo kutokana na maombi ya Kamati ya Ligi kwa vile baadhi
ya wajumbe wa Baraza la Bodi hiyo kuwa vilevile wajumbe wa Mkutano Mkuu
wa TFF.
TFF
itafanya Mkutano Mkuu wake Oktoba 26 mwaka huu ambao utakuwa na ajenda
za kawaida kama zilivyoainishwa katika Katiba yake wakati ajenda ya
uchaguzi itakuwa Oktoba 27 mwaka huu.
Wagombea
uongozi TPL Board ni Hamad Yahya Juma anayewania nafasi ya Mwenyekiti
wakati Makamu Mwenyekiti ni Said Muhammad Abeid. Wanaowania nafasi za
ujumbe katika Kamati ya Uongozi ni Kazimoto Miraji Muzo na Omar Khatib
Mwindadi.
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu Mbwezeleni
inatarajia wakati wowote kutangaza tarehe ya kuanza kampeni kwa wagombea
katika uchaguzi huo. Baraza la Bodi linaundwa na wajumbe 38 ambao ni
wenyeviti 14 wa klabu za Ligi Kuu na wenyeviti 24 wa klabu za Daraja la
Kwanza.
KAMATI YA JAJI LUANDA KUSIKILIZA RUFANI ALHAMISI
Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda
itakutana keshokutwa (Oktoba 10 mwaka huu) kusikiliza rufani
zilizowasilishwa mbele yake.
Waombaji
uongozi watatu wamekata rufani katika Kamati ya Jaji Luanda wakipinga
kutopitishwa kugombea katika uchaguzi wa TFF, uamuzi uliofanywa na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ajili ya uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba
27 mwaka huu.
Warufani
ni Samwel Nyalla aliyeondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji
kupitia Kanda namba 2 ya mikoa ya Mara na Mwanza kwa kutojaza kikamilifu
fomu namba 1 ya maombi ya kugombea uongozi TFF kwa kutoonesha malengo
yake.
Ayoub
Nyaulingo yeye anapinga kuondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya
Utendaji kupitia Kanda namba 6 (Katavi na Rukwa) kwa kutokuwa na uzoefu
uliothibitika wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.
Naye
Ayoub Nyenzi amekata rufani kupinga kuondolewa kugombea ujumbe wa
Kamati ya Utendaji kuwakilisha Kanda namba 7 (Iringa na Mbeya) kwa
kushindwa kuthibitisha uraia wake.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment