MZUNGUKO WA VPL KUANZA JUMAMOSI
Mzunguko
wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara
unaanza Jumamosi (Januari 26 mwaka huu) kwa mechi tano katika miji ya
Bukoba, Dar es Salaam, Tanga wakati mechi ya Tanzania Prisons na Ruvu
Shooting inahamishiwa uwanja mwingine.
Ashanti
United itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Coastal Union itacheza
na Oljoro JKT katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Uwanja wa Azam
Complex, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Azam na Mtibwa
Sugar.
Jumapili
(Januari 26 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya JKT Ruvu na Mgambo
Shooting itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex wakati Simba na Rhino
Rangers zitaumana kwenye Uwanja wa Taifa.
Mechi
ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting iliyokuwa ichezwe Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine inahamishiwa uwanja mwingine kwa vile huo bado
nyazi zake ambazo zimepangwa hivi karibuni hazijawa tayari kuhimili
mechi hiyo.
Hivyo
Tanzania Prisons inatakiwa kutafuta uwanja mwingine unaokidhi viwango
vinavyotakiwa kwa ajili ya mechi hiyo, na nyingine dhidi ya JKT Ruvu
itakayochezwa Januari 29 mwaka huu.
Pia
matumizi ya tiketi za elektroniki yanaanza katika mzunguko huu kwa vile
viwanja nane ambavyo tayari vimefungwa vifaa vya tiketi hizo. Vilevile
tunakumbusha washabiki wa mpira wa miguu kuwa tiketi za elektroniki
haziuzwi viwanjani.
TWIGA STARS KUIVAA ZAMBIA FEB 15 LUSAKA
Tanzania
(Twiga Stars) itaivaa Zambia katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza
ya michuano ya mchujo ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itakayofanyika
Februari 15 mwaka huu jijini Lusaka.
Mechi
hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Nkoloma kuanzia saa 9 kamili kwa saa
za Zambia na itachezeshwa na mwamuzi Salma Mukansanga kutoka Rwanda.
Mukansanga
atasaidiwa na Wanyarwanda wenzake; Francine Ingabire, Sandrine Murangwa
na Angelique Tuyishime. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Jackey Gertse
kutoka Namibia.
KISHONGOLE, KESSY KUSIMAMIA MECHI ZA CAF
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua Watanzania Alfred Rwiza
Kishongole na Lina Kessy kuwa makamishna wa mechi za shirikisho hilo
zitakazochezwa wikiendi ya Februari 14 mwaka huu.
Kishongole
ameteuliwa kusimamia mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Cote d’Or
ya Shelisheli na Kabuscorp de Palanca ya Angola.
Mechi
hiyo ya marudiano ya raundi ya mchujo itafanyika Shelisheli na
itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Abdoul Ohabee
Kanoso. Waamuzi wengine ni Basile Alain Rambeloson, Augustin Gabriel
Herinirina na Andofetra Avombitana Rakotojaona.
Naye
Kessy atakuwa kamishna wa mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe
la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Rwanda na Kenya itakayochezwa
jijini Kigali.
Waamuzi
wa mechi hiyo wanatoka Cameroon. Mwamuzi wa kati ni Sylvie Abou wakati
wasaidizi wake ni Winnie li Koudangbe, Lum Rochelle na Jeanne Ekoumou.
No comments:
Post a Comment