Jamal Malinzi Rais wa TFF akimpa mkono wa kwaheri aliyekuwa kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen |
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen wamekubaliana
kuvunja mkataba katika makubaliano ambayo ni siri kwa pande zote mbili.
Uamuzi
huo umetangazwa leo (Februari 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa pamoja na
Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Kocha Poulsen mbele ya waandishi wa habari.
Rais
Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa shukrani za dhati kwa Kocha Poulsen kwa
ushirikiano na mchango ambao ameutoa kwa Tanzania kuanzia kwenye mpira wa miguu
wa vijana.
Naye
Kim amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi cha miaka
mitatu alichokaa nchini kuanzia Mei 2011 alipoteuliwa kuwa kocha wa timu za
Taifa za vijana, na baadaye Taifa Stars.
Akizungumzia
benchi jipya la ufundi la Taifa Stars, Rais Malinzi amesema linatarajiwa
kutangazwa hivi karibuni likiongozwa na kocha kutoka nje ya Tanzania.
Amesema
kwa upande wa mechi dhidi ya Namibia itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini
Windhoek, Stars itaongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi
akisaidiwa na kocha Hafidh Badru kutoka Zanzibar.
Katika
hatua nyingine, Kocha Madadi amewaondoa wachezaji watano wa Yanga katika kikosi
kilichotajwa awali ili wapate fursa ya kuitumikia timu yao kwenye mechi mbili
za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri.
Wachezaji
hao ni Athuman Idd, David Luhende, Deogratius Munishi, Frank Domayo, Kelvin
Yondani na Mrisho Ngasa. Pia kipa Ivo Mapunda ameondolewa katika kikosi hicho
baada ya kupata msiba.
Nafasi
zao zimezibwa na wachezaji Abdi Banda (Coastal Union), Himid Mao (Azam), Juma
Luizio (Mtibwa Sugar), Said Moradi (Azam) na Shabani Kado (Coastal Union).
Taifa
Stars itaingia kambini keshokutwa (Machi 1 mwaka huu) jioni kwenye hoteli ya
Accomondia jijini Dar es Salaam, na itaondoka Machi 3 mwaka huu alfajiri kwa
ndege ya South African Airways na kurejea nchini Machi 7 mwaka huu saa 8.15
mchana.
No comments:
Post a Comment