Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ya
Airtel Rising Stars, itayofanyika Jijini Nairobi, Kenya kuanzia Agosti 19 mpaka
25 wameanza maandalizi yao kwenye Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam.
Michuano hiyo ya vijana wenye umri chini ya miaka kumi na saba
itawaleta pamoja wachezaji takribani 500 kutoka nchi 15. Nchi hizo ni Uganda,
Malawi, DRC, Congo Brazzaville, Nigeria, Ghana, Zambia, Niger, Gabon, Burkina Fasso,
Sierra Leone, Chad, Madagascar, Tanzania na wenyeji Kenya.
Timu ya Tanzania itawakilishwa na wachezaji 16 waliochaguliwa
kwa kufanya vizuri kwenye michuano ya fainali ya taifa ya Airtel Rising Stars
iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume mwezi Juni mwaka huu.
Bingwa wa michuano hiyo, licha ya kutunukiwa nishani, atapewa
kombe na kupata fursa ya timu nzima kushiriki kwenye kliniki ya soka ya
kimataifa itakayofanyika Nairobi kwenye ya ukufunzi wa waalimu wa soka ya
vijana kutoka klabu za Manchester United na Arsenal za Uingereza.
Akiongea na waandishi wa habari kwenye Ofisi za TFF leo, Afisa
Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde alisema kampuni ya Airtel imeamua kufanya
kazi kwa karibu na chama cha Mpira wa miguu cha Dar es Salaam (DRFA) katika
kuvumbua vipaji vinavyochipukia.
‘Tunafuraha sana kwa mpango huu. Ninaamini wachezaji
watakaotuwakilisha kwenye hii michuano ya Bara la Afrika ya Airtel Rising Stars
huko Nairobi watatuletea heshima kubwa sisi Watanzania.’ Alisena Matinde.
Kikosi cha Tanzania kinaundwa na wachezaji wafuatao – Denis Richard,
Juma Hamza, Abdul Selemani, Ishaka Shekolowa, Bakari Ally, Abdulatif Mohamed,
George Joseph, Badilu Said, Said Kassim, Amos Ikungula, Paul Balama, Goodluck
Mabiku, Joel Kasimula, Ibrahim Mtenga, Sntkony Angelo na Suleiman.
Airtel Rising Stars ni mpango kabambe wa kuibua na kukuza vipaji
vya wanasoka wanaochipukia barani Afrika. Walengwa ni wavulana na wasichana
wenye umri chini ya miaka kumi na saba ambao watapata fursa ya pekee ya
kuonyesha vipaji vyao mbele ya wataalamu wa mpira wa miguu wa kitaifa na
kimataifa.
No comments:
Post a Comment