Mwanariadha wa Ethiopia Kenenisa Bekele alimuonyesha
kivumbi bingwa wa olimpiki Mo Farah kwa kumshinda katika mbio za Great
North Run.
Fara mwenye umri wa miaka 30 na mkimbiaji wa
Uingereza, alijitahidi kusalia mbele ya Bekele katika mita 400 za mwisho
lakini akapokonywa ushindi katika msitirati wa mwisho kwa sekunde moja.
Mkimbiaji mwingine wa Ethiopia,
Haile Gebrselassie, alimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuanza
kuchoka katika maili 13.1 za mwisho.
"Sijafurahia sana leo lakini nilimaliza wa pili
kwa mwanariadha shupavu.’’ Alisema Farah baada ya kumaliza kwa muda wa
saa moja na dakika kumi.
Farah na Bekele walimaliza kwa mtindo wa aina
yake kila mmoja akitaka kumaliza wa kwanza katika mashindano ya kufana
na ambayo yalisubiriwa kwa hamu kuu katika mtaa wa Newcastle hadi South
Shields.
Mabingwa hao watatu wa mbio, Farah, Bekele na
Gebrselassie – wanajivunia ubingwa wa dunia kila mmoja na ubingwa wa
olimpiki na walikimbia kwa karibu sana hadi Bekele, aliyekuwa anakimbia
nusu Marathon yake ya kwanza , kujitenga nao.
Upande wa wanawake, Mkenya Priscah Jeptoo nusura
avunje rekodi ya dunia baada ya kukimbia kwa kasi zaidi katika nusu
Marathon ya wanawake.
Priscah mwenye umri wa miaka 29, na mshindi wa
mbio za Marathon za London mwaka huu alichelewa tu kwa sekunde 5 kuweza
kuvunja rekodi iliyowekwa na mkimbiaji wa Uingereza Paula Radcliffe
miaka kumi iliyopita.
Meseret Defar alivunja rekodi ya Ethiopia alipochukua nafasi ya pili ingawa mbele ya Tirunesh Dibaba.
No comments:
Post a Comment